Raia wawili wa Uholanzi na vigogo wanne wa Wizara ya Maliasili na Utalii
wanaoshtakiwa kwa kutaka kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Armenia,
wamewasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.
Washtakiwa hao
waliofikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi
Aprili Mosi, walirudishwa mahabusu na kutakiwa kuwasilisha maombi hayo
Mahakama Kuu.
Sheria ya Uhalifu wa Kupangwa ikisomwa na kifungu
57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya 2002, inataka kesi ya
uhujumu uchumi kwa kosa linalozidi Sh10 milioni isikilizwe na Mahakama
Kuu.
Habari zilizothibitishwa na uongozi wa Mahakama Kuu Kanda
ya Moshi jana zilieleza kwa nyakati tofauti mawakili wa utetezi kutokea
jijini Arusha waliwasilisha maombi hayo juzi.
Waholanzi hao,
Artem Vardanyian (52) na Eduard Vardanyian (46) na Mtanzania Iddy
Misanya ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Arusha Birds Traders
wamefungua maombi namba 3/2016.
Washtakiwa wengine, Dk Charles
Mulokozi amefungua maombi namba 5/2016 wakati Nyangabo Musika (39),
Martina Nyakangara (34) na Very Anthony (33) wamefungua maombi namba
4/2016.
Dk Mulokozi ni Naibu Mkurugenzi wa Wanyamapori
(Rasilimali Endelevu), Nyakangara, Martina na Very ni maofisa wa Idara
ya Wanyamapori.
Mawakili wa utetezi, Robert Rogath, John Masangwa na
Alex Artem ambaye ni mtoto wa Artem, walionekana siku nzima juzi na jana
nje ya viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Moshi wakifuatilia maombi
hayo.
Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Bernard Mpepo
alithibitisha kupokelewa kwa maombi hayo na kwamba, yapo mezani kwa Jaji
Mfawidhi, Aishiel Sumari kwa hatua zaidi za kisheria.
Post a Comment