Askofu
mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la
Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa
Watawa Duniani imekuwa ni fursa kwa Familia ya Mungu kuandamana ili
kuwafahamu zaidi watawa wanaoendelea kushuhudia utajiri wa Injili katika
mazingira magumu na hatarishi; katika umaskini na hali ngumu za
kiuchumi; katika mahangaiko ya ndani, dhuluma na nyanyaso katika medani
mbali mbali za maisha ya binadamu.
Watawa ni mashuhuda
wa Injili, wanaojisadaka ili kuwaendea watu wanaoishi pembezoni mwa
jamii ili kuwaonesha utajiri wa Injili ya huruma ya Mungu. Watawa
wanaishi na kumwilisha Injili ya imani, matumaini, huruma na mapendo
kati ya watu wanaowazunguka, kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa
ajili ya Kristo na Kanisa lake kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za
dunia.
Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yamekuwa na mafanikio makubwa
katika maisha na utume wa Kanisa. Hii imekuwa ni hija ya watawa katika
maisha na utume wao, ili kuambata neema na huruma ya Mungu
inayowawezesha kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa
hata kama mbele yao kuna vikwazo na vizingiti kibao! Watawa wamepata
nafasi ya kutafakari kuhusu karama na roho ya mashirika yao, tayari
kuiendeleza kwa kusoma alama za nyakati.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko amewahamasisha watawa
kutoka huko kwenye “viota vyao” walikojificha, huku wakiwa na mwelekeo
mpya, waweze kuwa tayari kuwaendelea watu walioko pembezoni mwa jamii,
ili kuwashirikisha mambo makuu katika maisha yao. Maadhimisho haya
imekuwa ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu taalimungu ya maisha
ya wakfu, dhamana, wito na wajibu wao ndani ya Kanisa na Jamii katika
ujumla wake.
Familia ya Mungu imepata nafasi ya pekee kuweza kutafakari kwa kina
na mapana tunu msingi za maisha ya kuwekwa wakfu; maisha ya udugu ndani
ya jumuiya; utume wa watawa ndani ya Kanisa; ushuhuda wa maisha ya
kitawa katika huduma kwa familia ya Mungu hususan katika sekta ya elimu,
afya na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na
kimwili. Imekuwa ni nafasi kwa watawa kufahamu karama za mashirika mbali
mbali, tayari kushirikiana katika kutangaza na kushuhudia Huruma ya
Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya
huduma makini.
Kwa hakika imekuwa ni nafasi ya kumshukuru Mungu pamoja na kukuza
ukarimu na upendo kwa watawa kwani hawa ni kati ya mihimili mikuu ya
Uinjilishaji wa kina. Viongozi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya
Kitawa na Kazi za kitume wametembelea sehemu mbali mbali za dunia na
kushiriki katika warsha, makongamano na semina za kitaifa na kimataifa.
Huko wameshuhudia jinsi ambavyo vijana wanachangamkia maisha ya kitawa,
tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa kuambata
mashauri ya Kiinjili, yaani: Utii, Ufukara na Useja. Baraza la Kipapa
pia katika kipindi cha mwaka mzima limekuwa likitoa tafakari za kina
kuhusu umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha; Kusoma
Maandiko Matakatifu pamoja na Tafakari ya kina.
Kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya Baraza la Kipapa na Mabaraza
ya Maaskofu Katoliki katika kuhamasisha na kuadhimisha Mwaka wa Watawa
Duniani. Maadhimisho haya pia yamepata mwelekeo wa pekee katika
majadiliano ya kiekumene kwa kutambua kwamba, hata Makanisa mengine ya
Kikristo kuna watawa wanaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Watawa wameweza kufanya mkesha wa sala; watawa vijana wakakutana mjini
Roma ili kushuhudia ile furaha ya maisha wakfu kwa ajili ya Mungu na
jirani.
Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yamejikita katika Ibada,
Tafakari, Maungamo, Mwongozo wa maisha ya kiroho. Kilele cha maadhimisho
ya Mwaka wa Watawa Duniani ni kuanzia tarehe 28 Januari hadi tarehe 2
Februari, 2016 Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya
Watawa Duniani. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “ Maisha ya
wakfu katika umoja”. Hili ni tukio kuu kwa maisha na utume wa watawa
kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Baba Mtakatifu Francisko ndiye aliitisha Maadhimisho ya Mwaka wa
Watawa Duniani; akawasindikiza katika sala na sadaka yake;
akawatajirisha kwa njia ya upendo na tafakari za kibaba; akawaonya kwa
njia huruma na upendo wa Mungu. Tafakari zake zimekuwa ni utajiri mkubwa
kwa maisha na utume wa watawa sehemu mbali mbali za dunia. Ni matumaini
ya Kanisa kwamba, matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani
yatakuwa ni chachu ya maendeleo kwa sasa na kwa siku za usoni.
Kwa njia hii, watawa wataendelea kusonga mbele kwa ujasiri ili
kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha na utume wao kwa moyo wa
ujasiri pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kusikiliza na
kujibu kilio cha familia ya Mungu kwa nyakati hizi, daima wakimwachia
Roho Mtakatifu nafasi ya kuwaonesha dira na njia ya kufuata katika
maisha na utume wao.
Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yamekwenda sanjari na Mwaka
Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kukazia kwa namna ya pekee,
ufuasi wa Kristo wenye mashiko na mvuto; unaoshuhudia na kumwilisha
huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Watawa wanapaswa
kuwa ni kielelezo cha Msamaria mwema anayethubutu kujitoa mhanga ili
kuwaganga wale wanaoteseka kiroho na kimwili kwa njia ya huduma,
Sakramenti za Kanisa na faraja ya Neno la Mungu linaloshuhudiwa katika
matendo ya huurma: kiroho na kimwili. Bila Injili ya huruma ya Mungu,
maisha na utume wa watawa ni sawa na “daladala” iliyokatika usukani,
haina mwelekeo wana mashiko katika huduma kwa Mungu na jirani.
Kanisa linatambua na kuwathamini watawa wote kutokana na mchangao wao
katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa kuna haja ya kukuza na kudumisha
maisha ya sala, tafakari, udugu na umoja; mambo msingi yanayojenga na
kuimarisha maisha ya kitawa na kazi za kitume, kwani wote ni ndugu
katika Kristo.
Post a Comment