Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini Mhe.Jaji Francis Mutungi ameviasa Vyama vya Siasa kushiriki chaguzi
zinazotangazwa na tume za uchaguzi nchini ikiwemo uchaguzi wa Machi 20, mwaka
2016 uliotangzwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa kwa vyama hivyo leo na kusainiwa na Jaji Mutungi ilieleza kwamba, kimsingi Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya
258 inasisitiza vyama vya siasa kushiriki katika chaguzi zote zinazotangazwa
na tume za uchaguzi ili kufikia malengo yake ya kushika dola.
“Katika nchi
kidemokrasia na kwa chama cha siasa kinachoamini misingi ya kidemorasia ya
vyama vingi vya siasa, hakuna njia mbadala kwa chama cha siasa kufikia malengo
yake zaidi ya kushiriki uchaguzi.
“Ni wajibu wa kila
chama cha siasa nchini kama wakala wa
kukuza demokrasia, utawala wa sheria na amani ya nchi, kuwa wa kwanza kutii
matamko ya kisheria yanayotolewa na mamlaka husika . Kama kuna chama cha siasa hakiridhiki
au kimekwazwa kwa njia moja au nyingine na suala lolote kuhusu masuala ya
uchaguzi, njia stahiki na inayonyesha ukomavu wa kisiasa si kuhamasisha kugomea
uchaguzi, bali ni vema kikafuata utaratibu uliowekwa katika sheria za uchaguzi,”
alisema Jaji Mutungi.
Aidha Msajili huyo
amesema kwa mujibu wa Sheria za Nchi bado ni suala la hiari kwa chama kushiriki
uchaguzi lakini utashi huo wa hiari unaenda sanjari na umuhimu wa kila chama
kushiriki kila uchaguzi unaotangazwa na tume ya uchaguzi.
“Hivyo ni muhimu basi
kila chama cha siasa kuelewa kuwa,uchaguzi ni kipimo cha uhai wa chama cha
siasa. Chama cha siasa kisiposhiriki uchaguzi kinaua uhai wake katika mtazamo
wa harakati za kisiasa,” alisisitiza.
Aliongeza kwamba hivi
sasa, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na vyama vya siasa vimeimarika, hivyo
sio vyema kwa chama cha siasa kujirudisha nyuma au kujiua kisiasa kwa
kutoshiriki uchaguzi wakati kina uwezo wa kufanya hivyo.
Post a Comment