BREAKING NEWS

Saturday, 30 January 2016

Abasia ya Hanga Tanzania yapata Jembe la nguvu! P. Octavian Masingo, OSB.


Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani imekuwa ni fursa nyeti kwa Watawa wa Shirika la Mtakatifu Benedikto, Abasia ya Hanga iliyoko Jimbo kuu la Songea, Tanzania, kutafakari kwa kina na mapana kuhusu uongozi kama huduma ya udugu na mapendo katika maisha ya kuwekwa wakfu, tayari kumuiga Kristo mchungaji mwema aliyewafunulia watu huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwendelezo wa kupyaisha maisha ya kitawa kwa kujikita katika tunu msingi za kiinjili, katiba na kanuni msingi za maisha ya kitawa. Huu pia ndio mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anayewakirimia kiongozi kadiri ya mapenzi yake!

Hivi karibuni, Watawa wabenediktini wa Afrika, Abasia ya Hanga iliyoko Jimbo kuu la Songea Tanzania walimchagua Mheshimiwa Padre Octavian Thomas Masingo, OSB kuwa ni Abate wa tatu wa Abasia ya Hanga, Jimbo kuu la Songea. Abate mteule alizaliwa tarehe 27 Aprili 1975, Parokiani Dung’unyi, Jimbo Katoliki Singida. Baada ya masomo na malezi yake ya kitawa, kunako mwaka 2003 akaweka nadhiri zake za kwanza. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi kutoka Seminari kuu ya Peramiho, Jimbo kuu la Songea, akapewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 17 Juni 2010.
Abate mteule alitumwa kuendelea na masomo ya juu  Chuo kikuu cha Mtakatifu Augostini cha Tanzania, SAUT, kilichoko Jimbo kuu la Mwanza na kujipatia shahada ya kwanza katika fani ya Uongozi, kunako mwaka 2013. Wakati huu alipochaguliwa kuwa Abate, alikuwa anamalizia masomo yake katika uongozi ili kujipatia shahada ya uzamili toka SAUT, masomo ambayo anatarajiwa kuhitimu mwezi Julai, 2016.
Abate mteule Octavian anamrithi Abate Thadei Mhagama, OSB aliyeongoza kama Abate wa pili baada ya kupokea uongozi kutoka kwa “nguri” Abate Alcuin Nyirenda, OSB aliyeweka msingi thabiti wa uongozi wa Watawa Wabenediktini wa Afrika, leo hii wamekuwa kweli ni moto wa kuotea mbali, mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu unaojionesha katika maisha ya sala na kazi! Itakumbukwa kwamba, Abate Nyirenda ameongoza Abasia ya Hanga toka Mwaka 1994 hadi mwaka 2004 kipindi cha kazi na maendeleo makubwa.
Taarifa zinazonesha kwamba, wakati huu Abate mteule anapomalizia masomo yake huko SAUT, Mwanza, Abasia ya Hanga itakuwa chini ya uongozi wa Priori Jerome Mlelwa, OSB. Abate mteule baada ya kusimikwa katika tarehe itakayopangwa anatarajiwa kuanza rasmi utume wake hapo tarehe 1 Agosti 2016. Watawa wa Abasia ya Hanga Jimbo kuu la Songea wanamshukuru Mungu aliyewapatia kiongozi wakati huu wanapofunga Mwaka wa Watawa Duniani ili kuendeleza matunda yaliyopatikana kwa njia ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wanamwombea Abate mteule Octavian, linda na tunza ya Bikira Maria; busara na hekima ya Roho Mtakatifu, ili yote yawe ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, Baba mwenye huruma na mapendo.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree