Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye yupo
mapumzikoni nyumbani kwake Lubambangwe katika kijijini cha Mlimani,
Wilaya ya Chato Mkoani Geita, kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa
Rais, ameungana na waumini wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya
Chato, kusali ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka ambapo pamoja na mambo
mengine amewahusia watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili
liendelee kuwa na amani.
"Niwaombe watanzania wote tuendelee kushirikiana na kushikamana, kwa umoja wetu na siku zote tumtangilize Mungu mbele.
"Wakati
tunaadhimisha wiki moja baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo,
Yesu Kristo alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, sisi wote tujitahidi
kufuata matendo ya Yesu Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana
na tusibaguane" Amebainisha Rais Magufuli
Pamoja
na Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ibada hiyo imehudhuriwa
na Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Raila Amoro Odinga na Mkewe
Mama Ida Odinga, ambao ni familia rafiki wa Rais Magufuli, waliowasili
hapa Chato jana jioni Tarehe 02 April, 2016 kwa mapumziko wakitokea
Nairobi, Kenya.
Katika
salamu zake kwa waumini wa Parokia ya Chato, Mheshimiwa Odinga
amewashukuru watanzania kwa uhusiano mzuri walionao na wakenya, huku
akitoa mfano wa jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alivyojitoa kupigania uhuru wa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Kenya.
Mheshimiwa
Odinga ametoa mfano wake mwenyewe kuwa Mwalimu Nyerere alimpatia pasi
ya kusafiria ya Tanzania, aliyoitumia kwa miaka mitatu kwa ajili ya
kwenda kusoma nje ya nchi, baada ya utawala wa Kikoloni wa Kenya kukataa
kumpa pasi hiyo.
Kuhusu
urafiki wake na Rais Magufuli, Mheshimiwa Odinga amesema urafiki huo
ulianza tangu Rais Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na yeye
kuwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi wa Kenya, ambapo mara kadhaa
walibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango ya miradi ya
ujenzi wa barabara, na kwa umuhimu huo ametoa wito kwa nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki kuendeleza ushirikiano na mshikamano ulioasisiwa na
waasisi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania, Jalamogi Odinga wa
Kenya na Milton Obote wa Uganda.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
Post a Comment