Upande
wa madai katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa Nyamagana jana
ulifunga ushahidi baada ya Mahakama Kuu kukataa ombi la kutumia fomu
namba 21B kwa ajili ya mashahidi wengine.
Baada
ya kufunga ushahidi katika kesi hiyo namba 5/2015, mbunge wa zamani wa
jimbo hilo (Chadema), Ezekiah Wenje dhidi ya Stanslaus Mabula (CCM),
upande wa utetezi leo unatarajiwa kuwasilisha hoja iwapo nao unafunga
ushahidi au utaita mashahidi mahakamani.
Hatua
hiyo imekuja jana baada ya Jaji Kakusilo Sambo kukubaliana na pingamizi
lililowekwa na upande wa wajibu maombi wakipinga mleta maombi kutumia
fomu hizo katika ushahidi wake.
Katika
pingamizi la mawakili wa utetezi, Vicent Tangoh anayemuwakilisha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Constantine Mutalemwa anayemuwakilisha
Mabula, walidai mdai hakutoa fomu hizo kwa utetezi ili kuzihakiki kwa
muda mwafaka kama alivyoagizwa na Mahakama, hivyo hazistahili kutumika
mahakamani.
Upande
wa utetezi ulidai licha ya kutowasilisha fomu hizo kwa muda mwafaka,
pia mlalamikaji aliziwasilisha kwa kutumia vifungu tofauti bila kuieleza
Mahakama sababu za msingi za kutaka aruhusiwe kuzitumia kama kielelezo.
“Fomu
hizi ndizo kiini cha maombi haya na mdai alipewa siku 10 kuzikabidhi
kwa upande wa utetezi ili kuzihakiki na kuandaa hoja za majibu,
hakufanya hivyo na kushindwa kutoa sababu za msingi za kutofanya hivyo,” alidai wakili Tangoh.
Baada
ya Mahakama kukubaliana na pingamizi hilo, wakili wa Wenje, Deya Outa
aliomba kufunga ushahidi kwani hawataweza kuita shahidi mwingine
kutokana na ushahidi wao wote kutegemea fomu zilizokataliwa.
Jaji
Sambo alikubaliana na ombi hilo baada ya upande wa utetezi kutokuwa na
pingamizi na kuahirisha kesi hiyo hadi leo mawakili hao wa utetezi
watakapowasilisha hoja zao, iwapo wanafunga ushahidi au kuita mashahidi
kupinga ushahidi wa Wenje ambaye ni shahidi pekee wa upande wa
mlalamikaji.
Post a Comment