WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka wananchi wa
visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi Machi 20, 2016 ili waweze kupiga
kura kwa amani na utulivu bila kubughudhiwa na mtu yeyote.
Kitwanga
amesema kuwa ulinzi umeimarishwa na kuwataka wananchi visiwani humo
kujitokeza kwa wingi kuja kumchagua kiongozi wanaompenda siku ya
uchaguzi huo na watarejea nyumbani kwao salama mara baada ya kumaliza
kupiga kura.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na Maafisa
Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na baadaye
kuzungumza na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Waziri Kitwanga
alisisitiza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vimejiandaa vizuri na
wananchi waondoe shaka kwani hawatakubali vurugu ya aina yoyote itokee.
“Jitokezeni
kupiga kura siku ya uchaguzi kwani ni haki yenu, nawahakikishia usalama
upo na wa hali ya juu, asijitokeze mtu yeyote akawatisha kutokuja
kupiga kura, tumejipanga vizuri na lengo letu kubwa kabisa ni kuwalinda
wananchi,” alisema Kitwanga.
Hata
hivyo Waziri Kitwanga alisema hakuna mwananchi yeyote anayehama
kwakuogopa vurugu siku ya uchaguzi bali watu wanasafiri kwasababu
mbalimbali ikiwemo hiki ni kipindi cha maandalizi ya Sikukuu ya Pasaka,
baadhi ya wananchi wanaenda kula sikukuu maeneo mbalimbali nchini na
wengine wanasafiri kutokana na majukumu mbalimbali na sio wamekuwa
wakimbizi wakikimbia sehemu zao kama inavyoenezwa.
“Acheni
kusikia habari za mitaani amani ipo, jitokezi kupiga kura na hii habari
mnayosikia eti watu wameanza kuyakimbia makazi yao ni uzushi tu, hakuna
kitu kama hicho, wananchi wanaendelea na shughuli zako kama kawaida na
vyombo vya ulinzi vimejipanga kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na
mali zao,” alisema Kitwanga.
Waziri
Kitwanga aliwasili Zanzibar jana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya
kuimarisha usalama zaidi visiwani humo pamoja na kujua mikakati
iliyowekwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu usimamizi wa uchaguzi
huo.
Post a Comment