SIKU
moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kuteua wakuu wa mikoa wapya,
mtaalamu wa sayansi ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu, ameibuka na kusema
kuwa kuwapo kwa wanajeshi wengi wastaafu katika uteuzi huo
inadhihirisha wazi kuna dalili za utawala wa kijeshi nchini.
Profesa Baregu amesema kuwa wanajeshi huwa hawana hulka ya kidemokrasia.
“Kitu
kimoja kinachojitokeza kwenye uteuzi huu ni kuwepo kwa wanajeshi
wastaafu, na mimi ninavyoelewa wanajeshi huwa hawana hulka za
kidemokrasia. Hii inaonyesha wazi kwamba utawala huu ni wa kijeshi,” alisema.
Profesa
Baregu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), alisema haileti picha nzuri kuwapo kwa wanajeshi
wengi katika utawala kwa sababu tawala za mikoa na wilaya ni saula la
kiraia na demokrasia zaidi.
Alisema
rasimu ya katiba ambayo yeye alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ilipendekeza kupitia upya tawala za mikoa na
kupunguza idadi yake.
“Kutokana na hilo, mamlaka ya wananchi inamezwa kwa sababu wakuu wa mikoa na wilaya ni wengi na kunakuwepo na mgongano mkubwa,” alisema.
Kwa
upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru
Ali, alisema uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya ni wa rais na
wanaoteuliwa ni watu mchanganyiko.
Naye
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence
Mpangala, alisema kila anapoingia kiongozi mpya anaunda timu ambayo
anaona ataendana nayo.
Post a Comment