Thursday, 4 February 2016
Watu wanapaswa kufahamu ukweli ili kuponya madonda ya moyoni!
Posted by Unknown on 00:43:00 in | Comments : 0
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Februari 2016 amekabidhiwa nakala ya Kitabu cha “La Squadra Pontificia Dardanelli 1657” kilichochapishwa kwa lugha ya Kiitalia na Kituruki, mkusanayiko wa nyaraka mbali mbali kutoka katika Maktaba kuu la Vatican kuhusu mchango wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika vita ya pili ya Dardanalles kunako mwaka 1657.
Mtunzi wa kitabu hiki Bwana Rinaldo Marmara anasema lengo ni kuonesha mchango wa Maktaba kuu ya Vatican kwa ajili ya wanahistoria na watafiti kutoka Uturuki.
Hiki ni kitabu kinachoonesha machungu yaliyojikita katika historia, lakini pia kinaonesha mchango na juhudi za mwandishi wa kitabu hiki wa kutaka kufanya utafiti na uchunguzi wa kina kwa ajili ya huduma ya ukweli, tayari kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana, kushirikiana na kuelewana. Maktaba kuu ya Vatican imeendelea kuwa ni msaada mkubwa kwa watafiti na wachunguzi wa masuala ya kihistoria kutoka Uturuki, ili kwa pamoja waweze kuelewa matukio ya kihistoria yaliyosababisha mateso na mahangaiko kwa watu wasiokuwa na hatia, kama vile maafa ya mwaka 1915.
Kurasa chungu za historia ya watu hazipaswi kusahauliwa, bali kufanyiwa tafakari ili kukoleza mchakato wa uponyaji na usafishaji wa kumbu kumbu, mambo msingi yatakayowasaidia watu kuambata msamaha na upatanisho kati ya watu. Kitabu hiki kinamkumbuka pia Balozi Taha Carm aliyekuwa mwakilishi wa Uturuki mjini Vatican, aliyeuwawa kikatili na kikundi cha kigaidi kunako mwezi Juni 1977. Hii ni fursa pia ya kuendelea kulaani vitendo vyote vya kigaidi vinavyoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.
Mauaji na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa kwa misingi ya udini yanapaswa kukemewa vikali na kwamba waamini wa dini mbali mbali washikamane kwa pamoja kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko alikazia wakati wa hija yake ya kitume Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Changamoto ya Baba Mtakatifu Francisko iwe ni chachu ya kujenga na kudumisha udugu, mshikamano, huruma na utu, ili waamini wote kwa pamoja waweze kusimama imara kupinga vita na mauaji!
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment