BREAKING NEWS

Thursday, 4 February 2016

Haki ya Mungu ni Huruma yake!


Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea na Katekesi zake kama kawaida na Jumatano, tarehe 3 Februari 2016 ametafakari kuhusu huruma na haki ya Mungu kadiri ya Maandiko Matakatifu yanayomwelezea Mwenyezi Mungu kuwa mwingi wa huruma na haki timilifu. Lakini kwa bahati mbaya, mwanadamu anapotafakari juu ya huruma anajikuta mawazo yake yakiogelea katika masuala ya uongozi yanayotaka kulipa fidia na adhabu kutekelezwa.


Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, haki ya sheria za namna hii haziwezi hata siku moja kushinda maovu, bali maovu  yanafunikwa na kuendelea kuitesa jamii, kwani maovu yanashindwa kwa kutenda mema. Maandiko Matakatifu yanaonesha kwamba, haki ya kweli ni mchakato usiofumbatwa katika mwelekeo wa kimahakama. Haki inamwona mtu akielekea kutenda maovu na hivyo anapewa wito na mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu. Haki inawasaidia watu kuona maovu wanayotenda na hivyo kushtakiwa na dhamiri nyofu.
Kwa mwelekeo huu, watu waovu wanaweza kuona ubaya wao na hivyo kukimbilia huruma na msamaha wa Mungu. Hivi ndivyo familia zinapaswa kusamehe; kwa wanandoa na watoto wao kuoneshana upendo. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, jambo hili si rahisi sana kutendeka katika maisha ya kawaida, kwani linawataka waamini kusamehe na kutumainia wokovu wa wale waliowakosea. Hii ndiyo haki ya Mungu. Mwenyezi Mungu hana haja na hukumu ya watu wake, bali wokovu wa roho zao.
Watu kwa kuona makosa yao, Mwenyezi Mungu anawapatia neema ya kukimbilia huruma iliyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Haki ya Mungu anasema Baba Mtakatifu ni huruma yake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujianika mbele ya huruma ya Mungu na kuwa tayari kuwashirikisha huruma hii ndugu zao.
Baba Mtakatifu anaendelea kuwahamasisha watoto wa Mungu kuwa ni wamissionari wa huruma ya Mungu, kwa kupokea na kutoa msamaha kwa wengine, tayari kujipatanisha na jirani kwa kuanzia ndani ya familia. Sala ya Baba Yetu, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu, iwe ni changamoto kwa Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, tayari kumwita, Abba yaani Baba Yetu!
Papa ameishukuru kwa namna ya pekee familia ya Mungu Jimbo kuu la Trento kwa kutoa Mti wa Noeli, ambao umekuwa ni kivutio kikuu kwa waamini na mahujaji waliotembelea Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi ya kuimarisha imani inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree