BREAKING NEWS

Thursday, 4 February 2016

Papa afunga rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bwana kutolewa Hekaluni, sanjari na Siku ya 20 ya Watawa Duniani iliyoandamana na kuufunga rasmi Mwaka wa Watawa, hapo Jumanne tarehe 2 Februari, 2016 ameongoza maandamano ya watawa waliokuwa wamebeba mishumaa, kuashilia Kristo Mwanga wa Mataifa na baadaye akaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.


 Ibada ambayo imehudhuriwa na umati mkubwa wa watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amewakumbusha watawa kwamba, Sherehe ya kutolewa Bwana Hekaluni ni siku kuu ya watu kukutana, huu ni mwanzo wa maisha ya wakfu unaonesha ukaribu wa Mungu anayetaka kushirikiana na binadamu dhaifu na mdhambi, changamoto na mwaliko kwa watawa kutunza ndani mwao hazina hii muhimu katika maisha na utume wa Kanisa, daima wakionesha moyo wa shukrani, hasa pale wanaposhiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Baba Mtakatifu anasema Mtoto Yesu aliyetolewa Hekaluni anawakirimia binadamu huruma na upendo wa Mungu na kwamba, Yesu Kristo ni Sura ya huruma ya Baba wa milele. Hii ndiyo picha inayotolewa na Mama Kanisa wakati wa kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, tayari watawa kujisadaka na kujitoa kimasomaso kumezwa katika bahari ya Fumbo la Upendo wa Mungu unaosherehekewa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, hii ni Siku kuu ya watu mbali mbali kukutana, kwani katika Hekalu, Yesu anawaijia watu wake na watu wanamwendea. Mzee Simeoni anawakilisha Agano la Kale na matarajio ya Waisraeli wakati huu ahadi za Manabii zinapopata utimilifu wake. Nabii Ana binti ya Fanueli anapomwona Mtoto Yesu anajawa furaha na kuanza kumtukuza Mungu. Mzee Simeoni na Anna wanaonesha matumaini na unabii na kwamba, Yesu ni kielelezo cha mambo mapya na utimilifu wa maajabu ya Mungu. Kwa njia ya Yesu, watu wanaweza kukutana na yale ya kale katika kumbukumbu na ahadi pamoja na kuonja yale yajayo yanayosheheni matumaini.
Baba Mtakatifu Francisko anawaambia watawa kwamba, wao wanaitwa kuwa madaraja ya watu kukutana na kwa njia ya neema wanaweza kuwa na mwono mpya wa maisha. Kwa mtu ambaye amekutana kweli na Yesu katika hija ya maisha yake, ameonja mabadiliko ya dhati, kwani ni chachu ya mambo mapya na mtu anayeishi katika mwelekeo huu anakuwa ni shuhuda ambaye anawawezesha watu kukutana, tayari kuhamasisha utamaduni wa watu kukutana, bila ya kujitafuta wenyewe hali inayoweza kuwapeleka kujifungia katika ubinafsi wao.
Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Yesu kwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti aliamua kujitwalia hali ya ubinadamu na kwamba, watawa kwa namna ya pekee wanaitwa kuwa ni mashuhuda amini na wa kinabii wa uwepo wa Mungu karibu ili kuweza kushirikiana na binadamu katika udhaifu, dhambi na mapungufu yake ya kibinadamu. Watawa wanaitwa kushiriki kikamilifu utume katika furaha na matumaini; katika majonzi na mateso ya watu wa nyakati hizi, hususan maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Kwa namna ya pekee watawa, wanahimizwa kutunza ndani mwao ule mshangao na upya wa maisha ya kiroho pasi na kuzama katika mazoea na utekelezaji wa karama zinazoelea katika ombwe, bali karama zinazomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa; kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha ya kitawa na kazi za kitume. Kamwe watawa wasiogope kwani wamekwisha kutana na Yesu aliyewakirimia neema na kuwalisha kwa tunu msingi za Kiinjili, tayari kumpeleka Kristo Yesu kwa watu wa mataifa kama walivyofanya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu kwa kumpeleka Mtoto Yesu Hekaluni. Watawa wanahamasishwa kufanya maamuzi magumu na ya kinabii katika maisha yao.
Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni ni mwaliko kwa waamini wote kuwa na moyo wa shukrani kama Ekaristi. Watu wawe na moyo wa shukrani kwa watawa ambao wamesadaka maisha yao kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa. Huu ndio muhtasari wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Shukrani kwa zawadi ya Roho Mtakatifu anayeliongoza na kulijalia Kanisa karama mbali mbali. Watawa waendelee kumwomba Bikira Maria ili awasaidie kukuza na kudumisha ile kiu ya kutaka kukutana, kuhifadhi mshangao na furaha ya shukrani, ili hatimaye, wakiongozwa na mwanga angavu waweze kukutana na Huruma ya Baba!

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree