Thursday, 4 February 2016
Dhamana na utume wa Balozi wa Vatican
Posted by Unknown on 00:52:00 in | Comments : 0
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa safari yake ya kikazi nchini Slovenia, Jumatano tarehe 3 Februari 2016 amezindua Jengo la Ubalozi wa Vatican nchini Slovenia pamoja na kushiriki maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 tangu Slovenia ilipojipatia uhuru wake. Tangu wakati huo nchi hii imekuwa na mchango mkubwa katika medani mbali mbali za kimataifa pamoja na kuchangia kudumisha na kuendeleza Mapokeo ya Kikristo kwa kujikita katika elimu na urithi wa kitamaduni.
Slovenia ilijipatia uhuru wake kunako tarehe 13 Januari 1992 na tarehe 8 Februari 1992 ikaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Kunako mwaka 1996 na 1999 Mtakatifu Yohane Paulo II akatembelea nchini humo, hija ya kitume ambayo imeacha chapa ya kudumu katika akili na mioyo ya watu wa Slovenia. Kunako mwaka 2004 mahusiano kati ya nchi hizi mbili yakaboreshwa zaidi kwa kutiliana sahihi itifaki ya makubaliano ya kisheria na kwamba kuna matumaini makubwa ya kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili.
Vatican ina mahusiano ya kidiplomasia yanayovuka mipaka ya kijiografia kwa kuzingatia sheria za kimataifa na itifaki za kidiplomasia. Tangu uwepo wa nchi ya Vatican, ilipewa haki ya kidiplomasia na kwamba, Vatican ni kati ya nchi ambazo zimekuwepo kwenye medani za kimataifa kwa miaka mingi. Lengo na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili. Vatican iko mstari wa mbele katika kudumisha Injili ya familia inaofumbata Injili ya uhai; tunu msingi zinazotishiwa na utamaduni wa kifo kwa nyakati hizi.
Balozi za Vatican ni wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika mchakato wa kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na Makanisa mahalia. Katika nchi husika, Ubalozi wa Vatican unalenga pamoja na mambo mengine kuwa ni kiungo muhimu kati ya Serikali na Kanisa mahalia sanjari na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Vatican daima iko makini kusikiliza kilio na matumaini ya Makanisa mahalia, ili kwa pamoja kusimama kidete kulinda na kutetea: haki msingi za binadamu, uhuru wa mawazo pamoja na uhuru wa kidini pamoja na kutekeleza dhamana utume wake kadiri ya sheria za nchi.
Kanisa Katoliki nchini Slovenia liko mstari wa mbele katika huduma ya elimu, afya na maendeleo endelevu na kwamba, Makao makuu ya Ubalozi wa Vatican nchini humo yatasaidia kuimarisha uelewano na ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa mahalia. Vatican inapenda kuwashukuru viongozi wa Serikali ya Slovenia kwa ushirikiano uliowezesha kukamilisha ujenzi wa Ubalozi wa Vatican nchini humo. Hiki ni kielelezo cha mshikamano na mshikamano; mahali pa watu kukutana na kushirikiana kwa ajili ya mafao ya wengi.
Kwa namna ya pekee, Kardinali Parolin amempongeza Askofu mkuu Julius Janusz, ambaye ni Dekano wa Wanadiplomasia kwa kazi makini ya ujenzi wa balozi mbali mbali huko Msumbiji, Hungaria na sasa Slovenia. Balozi wa Vatican hana budi kuonesha uwezo wa kujenga na kudumisha mahusiano kati ya watu kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi ili kugusa na kutafuta majibu ya pamoja yanayomwandama mwanadamu. Na huu anasema Kardinali Parolin ndio wito na dhamana ya kila Mkristo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment