Monday, 22 February 2016
Wadau wa habari saidieni kudumisha umoja wa kitaifa!
Posted by Unknown on 23:06:00 in | Comments : 0
Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini wanawaalika waandishi na wadau mbali mbali wa vyombo vya mawasiliano ya jamii kutekeleza vyema wajibu na dhamana yao ndani ya jamii ili kujenga na kudumisha: haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, ili Sudan ya Kusini iweze kusonga mbele kwa maendeleo endelevu na kuvukwa mkwamo wa kisiasa na kijamii ambao umekuwa na athari kubwa kwa maisha ya watu wengi.
Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni la Askofu msaidizi Santo Loku Pio wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini, wakati wa maadhimisho ya Miaka 10 tangu Kituo cha Radio cha Bakhita kilipoanzishwa katika eneo anamotoka Mtakatifu Josephine Bakhita. Wadau wa habari wawe makini katika taarifa zao, kwa kutambua na kudumisha utu, heshima na mafao ya wengi. Ni mwaliko wa kuondokana na sera za ubaguzi zinazojikita katika: upendeleo, ukabila na udini; mambo yanayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao ndani na nje ya Sudan ya Kusini.
Radio Bakhita ni matunda na juhudi za Wamissionari wa Comboni waliotaka kuhakikisha kwamba, Kanisa nchini Sudan linatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari kwa ajili ya Uinjilishaji wa kina unaomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa mara ya kwanza Kituo cha Radio cha Bakhita kilianza kurusha matangazo yake hapo tarehe 24 Desemba 2006 na kuanzia tarehe 8 Februari 2007 kikaanza kurusha matangazo haya kila siku, ili kuwapatia wananchi jukwaa la kujisikia na kujitambua kuwa ni sehemu ya Jamii na Kanisa na kwamba, wanakabiliwa na changamoto ya upatanisho, haki na amani; chachu ya maendeleo endelevu kwa jamii yoyote ile. Mbele ya wananchi wa Sudan ya Kusini, upatanisho, msamaha na umoja wa kitaifa ni mambo msingi ikizingatiwa kwamba, bado wananchi wengi wana madonda na majeraha makubwa ya vita na kinzani za kikabila na kisiasa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment