Monday, 22 February 2016
Makanisa yapongeza mkutano kati ya Papa na Patriaki Kirill wa Moscow!
Posted by Unknown on 23:04:00 in | Comments : 0
Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC limepokea kwa mikono miwili, tukio la kiekumene lililowakutanisha hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima, wakati huu dunia inapoendelea kushuhudia madhara ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, inayosababisha mateso na mahangaiko ya watu wengi. Ni matumaini ya Dr. Olav Fykse Tveit kwamba, mkutano na Tamko la Kichungaji lililotolewa na viongozi hawa wawili, litasaidia katika harakati za kutafuta na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni limefurahia hatua hii ya viongozi hawa wawili kukutana ili kuanza mchakato wa upatanisho wa kiekumene ili kganga na kuponya madonda ya utengano ambao umedumu kwa karne nyingi na hivyo kusababisha kunyong’onyea kwa ushuhuda wa imani ya Kikristo kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Majadiliano kati ya Papa Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow na Russia nzima ni kielelezo makini cha hamu ya kutaka kukuza na kudumisha umoja wa Wakristo, alama ya matumaini mapya, hususan wakati huu ambapo amani kwa mataifa mengi iko mashakani hasa huko Mashariki ya Kati na Ukraine.
Mambo yote haya yanasababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kiasi kwamba, leo hii kuna umati mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha! Ni matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, majadiliano haya yatakuwa kweli ni chachu ya mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendeleza juhudi zake, ili kweli amani na usalama viweze kupatikana katika maeneo ambayo bado yanakumbwa na migogoro ya kivita na mipasuko ya kijamii.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment