Monday, 22 February 2016
Familia ya Mungu Afrika Magharibi inajadili changamoto zake!
Posted by Unknown on 23:03:00 in | Comments : 0
Uinjilishaji mpya na changamoto maalum kwa Kanisa, familia ya Mungu Afrika Magharibi: Upatanisho, maendeleo na familia ndiyo mada inayochambuliwa na wanachama wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, RECOWA, CERAO, katika mkutano wake unaoanza tarehe 22 Februari, Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro Mtume na kuhitimishwa hapo tarehe 29 Februari 2016. Huu ni mkutano unaowashirikisha viongozi wakuu wa Kanisa kutoka katika nchi 15 za Afrika Magharibi. Mkutano huu unawashirikisha pia viongozi wa Serikali, dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Lengo ni kuangalia changamoto hizi katika mwelekeo mpana zaidi wa kidini na kiekumene; kisiasa na kijamii, ili hatimaye, kuibuka na mbinu mkakati kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Afrika Magharibi.
Huu ni mkutano wa pili kufanywa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, RECOWA, CERAO, lililoundwa kunako mwaka 2009, kwa kuyaunganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi yaliyokuwa yanazungumza lugha ya Kiingereza na yale yaliyokuwa yanatumia lugha ya Kifaransa. Mkutano wa kwanza wa Shirikisho hili uliofanyika kunako mwaka 2012, ulipembua pamoja na mambo mengine kuhusu “Familia ya Mungu Afrika Magharibi katika huduma ya upatanisho, haki na amani”.
Hii ilikuwa ni tafakari ya kina kuhusu changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Dhamana ya Afrika kwa kuitaka Familia ya Mungu Barani Afrika kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko wa kufanya yote mapya Barani Afrika kwa kuhakikisha kwamba, mchakato wa upatanisho, haki na amani unajikita katika wongofu wa ndani kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa binadamu, maridhiano; kwa kujali na kuheshimu Injili ya uhai. Kanisa Barani Afrika linahamasishwa kushirikiana kwa dhati kwa kuendelea kuinjilisha na kujiinjilisha kwa kukazia Maandiko Matakatifu, Sakramenti za Kanisa; yote haya ni kwa ajili ya Uinjilishaji mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumbe, mkutano wa sasa ni mwendelezo wa tafakari mintarafu changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa Uinjilishaji mpya Afrika Magharibi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment