JESHI
la Polisi Zanzibar limetoa tahadhari kwa watumiaji wa mitandao ya
kijamii ambao wanaitumia kwa kuwatukana viongozi wa kitaifa, huku likiwa
na orodha ya watu 34 ambao wanatarajiwa kuhojiwa zaidi kutokana na
matumizi mabaya ya mitandao hiyo.
Kauli
hiyo imetolewa juzi na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar
(DCI), Salum Msangi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika
Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
Alisema
hivi sasa baadhi ya watu wanaitumia mitandao hiyo kinyume na maadili
jambo ambalo linaweza kusababisha chuki na uhasama na kwamba ni kinyume
na maadili ya wananchi wa Unguja na Pemba.
Msangi
alisema jeshi hilo linakusudia kuwahoji watu 34 wanaotumia mitandao
hiyo ya kijamii kwa kuhamasisha vurugu pamoja na kutoa lugha za matusi
kwa viongozi wa Zanzibar, jambo ambalo ni kinyume na sheria pamoja na
utamaduni wa wananchi wa Zanzibar.
Alisema
mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba
25, mwaka jana, kumejitokeza baadhi ya watu na vikundi mbalimbali
vinavyotumia mitandao ya kijamii kwa kuandika maneno ya matusi au kutoa
video za kuzungumza zenye lugha ya matusi kwa kuwatukana watu mbalimbali
hasa viongozi wa kitaifa.
“Tayari
orodha ya watu hao imeshapatikana na hadi sasa Polisi inamshikilia kwa
mahojiano na uchunguzi mtu mmoja ambaye anatuhumiwa kutoa moja ya video
hizo zenye lugha ya matusi dhidi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein,” alisema.
Aidha
alisema kuwa uchunguzi wa kitaalamu na kisayansi unaendelea na
ukishakamilika jalada litafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa
ajili ya kulisoma na kulifikisha kwenye hatua zinazofuata.
Msangi
alitoa tahadhari kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwani
kutumia lugha za matusi ni kosa lililoainishwa kisheria kwenye sheria ya
kanuni ya adhabu, yoyote atakayetenda kitendo hicho atakamatwa na
kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, bila ya kujali limetolewa mahali
gani au wakati gani.
Hata
hivyo alisema kuwa wapo watu wanaodhani kuwa demokrasia ni uhuru wa
kuwatukana viongozi, jambo ambalo sio sahihi na halikubaliki kisheria na
kinyume na maadili ya wananchi wa Tanzania ambao wamejengwa na
utamaduni wa kuheshimu watu.
Msangi
ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Polisi Zanzibar, alisema orodha ya
watu wanaojiuhusisha na vitendo hivyo wanayo na wataendelea kukamatwa
mmoja baada ya mwingine na kuchukuliwa hatua zinazofaa kwa mujibu wa
sheria.
Hivi
karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria, Rais wa Zanzibar Dk
Ali Mohamed Shein alikemea tabia iliyojitokeza sasa ya matumizi mabaya
ya mitandao.
Post a Comment