Ujambazi
wa kutumia vifaa vya kivita umeibuka jijini Dar es Salaam, ukiwemo
uliofanyika katika uporaji wa Benki ya Access juzi, ambako majambazi
walitumia bunduki za kivita aina ya SMG na mabomu ya kurusha kwa mkono.
Akizungumza
jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro,
alisema mbali na uvamizi huo, pia Polisi imebaini na kukamata askari
bandia, waliokuwa na sare rasmi za Jeshi la Polisi zenye vyeo na redio
call, zenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya askari Polisi.
Akizungumzia
matukio hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga
alisema atakutana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk
Hussein Mwinyi, ili Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la
Polisi, waanzishe msako wa pamoja dhidi ya wahalifu hao.
Uvamizi, mauaji Mbagala
Akisimulia
ujambazi uliofanyika katika Benki ya Access Tawi la Mbagala, Kamanda
Sirro alisema majambazi hao walikuwa 12, wakiwa wamepakizana kwenye
pikipiki sita na walifika kwenye benki hiyo saa 8:30 mchana.
Baada
ya kufika, moja kwa moja waliingia kwenye chumba cha askari wanaolinda
benki na kumpiga risasi kichwani askari mwenye namba H7739 Konstebo
Harid na kufa papo hapo.
Mbali
na mauaji hayo, Kamanda Sirro alisema walimshambulia askari mwingine,
Konstebo Shaban miguuni na kupora silaha zao na kuingia nazo ndani ya
benki, ambako walimshambulia mlinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi na raia
wengine wawili na kufa papo hapo, huku wengine watano wakijeruhiwa.
Baada
ya hapo kwa mujibu wa Kamanda Sirro, majambazi hao walikimbilia chumba
kinachohifadhi fedha nyingi (strong room) na kukipiga risasi katika
jitihada ya kutaka kuingia ndani, lakini hawakuweza kuvunja.
Kutokana
na ugumu wa kuvunja chumba hicho, Kamanda Sirro alisema haraka haraka
wakahamia katika kaunta za watoa fedha na kupora fedha zilizokuwepo kati
ya Sh milioni 20 mpaka Sh milioni 30 na kuondoka na silaha za polisi
aina ya SMG mbili na ile yao moja pamoja na pikipiki zao.
Polisi waua watatu
Kamanda Sirro alisema taarifa zilisambazwa katika vikosi vya ulinzi, ambavyo vilijiimarisha.
Alitaja
Kikosi cha Mbwa na Farasi eneo la Mkuranga, ambao walijiandaa na
majambazi hao walipofika kijiji cha Chui wilayani Mkuranga mkoani Pwani,
walipambana na polisi na askari wakafanikiwa kuua majambazi watatu.
Mbali
na kuua watatu, silaha tatu zilikamatwa ambazo ndio zile SMG mbili za
Polisi, walizochukua pamoja na ile yao moja, lakini wakakutwa pia na
mabomu matatu ya kutupa kwa mkono yaliyotengenezwa Urusi.
“Hawa
majambazi walikuwa wamejiandaa, kwa maana walikuwa na mabomu ya kutupwa
kwa mkono matatu aina ya RGD 01 ambayo ni mbinu ya kujilinda
wanaposhambulia,” alisema Kamanda Sirro.
Tisa watoroka
Pamoja
na kujiimarisha kwa polisi, majambazi tisa walikimbia wakaacha pikipiki
zote sita za aina tofauti, ambazo ni Haojue mbili zenye namba MC 560
AED na MC 207 BAN, San LG yenye namba MC 784 BDJ, Boxer yenye namba MC
248 AXE na King Lion mbili zenye namba MC 653 BDQ na MC 853 BDR.
Kamanda
Siro alisema baada ya hapo, waliendelea kuwakimbiza majambazi hao hadi
wakatokomea katika Msitu wa Kongowe, ambako juhudi za kuwatafuta
zilianza mara moja.
“Nawahakikishia
wananchi mtandao wote wa ujambazi kwenye mabenki na maeneo mengine,
tutausafisha wote kwa maana hawa wanafanya uhalifu maeneo ya Dar es
Salaam na Pwani na wana ndugu zao, tutawakamata wote,” alisisitiza
Kamanda Sirro.
Alisema hawawezi kuona Watanzania wakiumia na kufa kwa tamaa za wachache, wenye kupenda utajiri wa haraka.
JWTZ kazini
Akizungumza
kuhusu ujambazi huo, Waziri Kitwanga alisema Polisi inajipanga upya na
atazungumza na Waziri mwenzake, Dk Mwinyi kuangalia jinsi ya majeshi
hayo mawili, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
watakavyofanya kazi pamoja ya msako katika misitu yote inayozunguka
mikoa ya Pwani, kuanzia Bagamoyo hadi Kisarawe.
Alionya kama kuna kambi za uhalifu ndani ya misitu hiyo, zitasambaratishwa na kuomba raia wema watoe taarifa za uhalifu.
“Tutafanya
operesheni kubwa na tutaifanya haraka, tunaomba wananchi watoe
ushirikiano hasa waendesha bodaboda kwa maana zinatumika sana kwenye
matukio haya. Mtandao wa majambazi ufahamu kwamba vyombo vya usalama
havijalala, tutawamaliza wote, tutatumia nguvu zetu zote kuwamaliza na
tutafanikiwa,” alisisitiza Kitwanga.
Kuhusu
waendesha bodaboda, Kitwanga alisema ukaguzi wa kina unafanywa na
kuwataka waendesha bodaboda hao wanaposimamishwa, wakubali na kutoa
ushirikiano na wasione kama wanabughudhiwa, bali ni kuwakagua kwa sababu
wahalifu hutumia vyombo hivyo zaidi kufanya matukio mabaya.
Polisi feki
Katika
tukio jingine, Kamanda Sirro alisema polisi feki wanne wamekamatwa na
wanashikilia kwa mahojiano, ili kubaini mtandao huo ambao unatumia sare
za Polisi, redio za upepo na pingu kufanya matukio ya uhalifu.
Alisema
walipata taarifa kutoka kwa raia wema ya kuwepo kwa mtandao wa askari
bandia, ambao hutumia sare za jeshi hilo kufanya matukio ya uhalifu,
ndipo walipowakamata hao wanne.
Kwa
mujibu wa Kamanda Sirro, polisi feki watatu walikamatwa Februari 24,
asubuhi saa mbili eneo la Upanga karibu na Daraja la Selander.
Alisema
watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, walikiri kufanya matukio ya ujambazi
kwa kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja anayeishi
Kinyerezi.
Kamanda
Siro alisema Polisi walimfuata mtuhumiwa huyo nyumbani kwake Kinyerezi
na walipofanya upekuzi, walimkuta na sare halisi ya Polisi, redio ya
upepo na pingu.
Kamanda
Sirro alisema baada ya uchunguzi, imebainika kwamba watuhumiwa hao
wamekuwa wakitumia sare na vifaa hivyo vya Polisi, kufanya matukio
mbalimbali ya ujambazi kwa kujiaminisha kuwa wao ni askari Polisi.
Alisema
watuhumiwa hao wamekiri kufanya matukio mbalimbali, ikiwemo kuweka
vizuizi katika barabara za mikoani na kufanya uporaji.
“Watuhumiwa
hao wote wanahojiwa ili waeleze jinsi walivyopata sare na vifaa hivyo
ya Polisi, wamekiri kufanya uhalifu maeneo mbalimbali, lakini wakati
mwingine tunashindwa kukamata wahalifu kwa sababu redio call wanayotumia
zinaingiliana na zetu, hivyo wanakuwa wamepata taarifa,” alisema
Kamanda Sirro.
Katika
tukio lingine, Februari 18 mwaka huu, watuhumiwa watatu wa ujambazi,
walikamatwa eneo la Kiwalani Kwa Mkude jijini Dar es Salaam wakiwa na
bastola moja.
Post a Comment