BREAKING NEWS

Thursday, 11 February 2016

Papa Francisko na Patriaki Kirill wa Moscow kuwasha moto wa kiekumene!



 Kardinali Peter Erdo’ Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, Ccee anasema, wamepokea kwa imani na matumaini makubwa taarifa ya mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Kirill wa Mosco na Rusia nzima, hapo tarehe 12 Februari 2016 huko Havana, Cuba kuwa ni hatua muhimu sana katika kukuza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kujenga umoja wa Kanisa. Hili ni tukio la kihistoria linalopania pamoja na mambo mengine kuwasha moto wa majadiliano ya kiekumene ambao umeendelea kwa miaka mihngi kufuka moshi.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya limekuwa likishirikiana bega kwa bega na Askofu mkuu Ilarione Volokolamsk, Rais wa Idara ya mahusiano ya Makanisa ya nje kutoka Upatriaki wa Mosco. Kwa njia hii wakafanikiwa kujenga jukwaa la majadiliano ya kiekumene Barani Ulaya kati ya Wakristo na Waorthodox, ili waweze kushirikiana kwa pamoja na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kwa sasa wanaandaa mkutano wa tano wa jukwaa la majadiliano kati ya Makanisa haya mawili. Tukio hili litasaidia mchakato wa kuimarisha majadiliano ya kiekumene ili wakristo kwa pamoja waweze kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko.
Kardinali Erdo’ anaendelea kufafanua kwamba, huu ni ujasiri unaoendelea kushuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, kwa kutaka kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na hivyo kuondokana na vikwazo ambavyo vimewatenga watu kwa misingi ya imani, siasa na tamaduni zao.
Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba linawapongeza viongozi hawa wakuu kwa kufanya maamuzi machungu katika historia na maisha ya Kanisa. Baada ya miaka mingi ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza” na kutoaminiana, sasa wameonesha ujasiri na ukomavu, utakaosaidia kusongesha mbele majadiliano ya kiekumene na kidini kati ya waamini wa dini na madhehebu mbali mbali.
Haya ni matunda ya kazi na mikono ya Baba Mtakatifu Francisko anayependa kujenga na kuimarisha utamaduni wa watu kukutana, kujadiliana na kujipatanisha, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu. Hizi ni juhudi wanasema Maaskofu Katoliki Cuba ambazo zimeiwezesha Cuba na Marekani kuweza kurejesha tena mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili zilizokuwa zinaonana kama “Paka na Panya; moshi na pua”! Huu ndio mwelekeo wa Baba Mtakatifu wa kushiriki pia maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani.
Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè imepokea taarifa hii kwa moyo mkuu na kuwataka wakristo kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa amani katika familia ya binadamu. Enzo Bianchi kwa upande wake anasema mkutano kati ya viongozi hawa wakuu wa Makanisa ni changamoto ya utii wa Injili ya Kristo inayowataka Wakristo wote kutafuta, kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa unaopata chanzo na hitimisho lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maahusiano kati ya Roma na Moscow yanakuwa ni kielelezo na mfano wa kuigwa kutokana na majadiliano ya kina yaliyofanyika kwa njia ya utakatifu wa maisha na hatimaye, kukubaliwa kwa kujikita katika utii wa Kiinjili. Huu ni ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene unaotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree