BREAKING NEWS

Thursday, 11 February 2016

Kwaresima ni kipindi cha kujipatanisha na Mungu na jirani!


Waamini kwa kupakwa majivu, wanaalikwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, daima wakitambua kwamba wanahitaji huruma ya Mungu. Wamissionari wa huruma ya Mungu ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu wanaotumwa kuganga na kuponya majereha ya dhambi. Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko wa kumrudia tena Mungu kwa moyo wote kwa njia ya sala, upendo na kufunga kwani utambulisho wa Mkristo ni upendo unaohudumia na wala si uchoyo na ubinafsi.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya Majivu, tarehe 10 Februari 2016 wakati wa mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ambamo pia amewapatia mamlaka Wamissionari wa huruma ya Mungu kwenda duniani kote ili kuwaondolewa watu dhambi zao. Baba Mtakatifu anasema, Neno la Mungu linawahamasisha waamini kutubu na kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, kwa kutambua kwamba, kama binadamu wanaogelea katika dimbwi la dhambi. Kumbe, wanahitaji kuonja msamaha na kwa njia ya neema ya Mungu wanaweza kushinda dhambi, lakini jambo la msingi anakaza kusema Baba Mtakatifu ni waamini kujitambua kwamba, ni wadhambi na wanahitaji huruma ya Mungu. Hii ni hatua ya kwanza katika hija ya maisha ya Mkristo inayomwezesha kupitia kwa Kristo Yesu, Mlango wa huruma ya Mungu, ili kupata maisha mapya!
Baba Mtakatifu anaonya kwamba, wakati mwingine kuna kishawishi cha mtu kutaka kujifungia katika undani na ubaya wa moyo wake, kwa kujihesabia haki na kujilinganisha na watu wengine ambao kwake ni wabaya zaidi kuliko alivyo! Kishawishi cha pili ni aibu ya kutaka kufungua mlango wa siri zilizohifadhiwa katika sakafu ya moyo wa mwamini, mwaliko kwa waamini kutambua kwamba, wanapaswa kuachana na dhambi kwa kujijengea fadhila ya uchaji wa Mungu. Kishawishi cha tatu anafafanua Baba Mtakatifu ni kukimbia Lango la Huruma ya Mungu, pale mwamini anapojikuta akitopea katika dhambi na hatimaye kujikuta akiwa katika mazoea ya kutenda dhambi. Katika mazingira kama haya, mwamini anaweza kuondokana nayo kwa njia ya neema inayomwezesha kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Kristo anayewakirimia amani na utulivu wa ndani!
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Wamissionari wa huruma ya Mungu wamekabidhiwa dhamana na mamlaka ya kuwa ni vyombo vya huruma ya Mungu, ili kuwasaidia waamini kumfungulia Mungu malango ya mioyo yao; kuvuka kishawishi cha aibu na kuambata mwanga wa neema ya Mungu badala ya kuukimbia na kuendelea kutopea katika dhambi za mazoea. Mikono yao iliyopakwa mafuta isaidie kuwainua waamini kwa upendo na huruma ya kibaba, tayari kuganga na kuponya madonda ya dhambi!
Kipindi cha Kwaresima ni fursa makini ya kumkimbilia Mwenyezi Mungu, kwani kwa njia ya dhambi wamejikuta wakiwa mbali na Uso wa huruma ya Mungu, kiasi hata cha kupoteza imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kumpenda Mungu na jirani badala ya kukumbatia malimwengu yanayoendelea kuwatumbukiza katika utupu wa maisha ya kiroho. Kwaresima ni kipindi cha waamini kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayoganga na kuponya dhambi. Ni wakati wa sala, upendo na kufunga.
Baba Mtakatifu anafafanua kwamba; Sala inamwezesha mwamini kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu tayari kukutana na Mungu kwa kutambua kwamba, daima anahitaji huruma, upendo na uwepo wake endelevu, kwani Mungu ni asili ya maisha na wokovu wa binadamu. Waamini wakati wa Kwaresima wajenge utamaduni wa kutenda mema kwa jirani kwa kuwaonjesha upendo unaojikita katika urafiki na huduma ili kushinda kishawishi cha kudhani kwamba, mtu anaweza kujitosheleza binafsi. Kwaresima ni kipindi muafaka cha kufunga na kujinyima, tayari kujikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kupata kile kilicho chema na uhuru wa kweli!
Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Kwaresima ni kipindi kilichokubaliwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumrudia Mungu kwa mioyo yao yote! Ni wakati wa sala, upendo, toba na wongofu wa ndani kwa kuondokana na unafiki katika maisha; hali ya kutojali shida na mahangaiko ya wengine. Ni wakati wa kusafisha nyoyo na maisha, ili kuambata utambulisho wa Kikristo unaojikita katika upendo unaohudumia, ili kushinda ubinafsi. Hii ni hija ya toba ya pamoja kama Kanisa kwa kupakwa majivu ili kuwakumbusha waamini kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi, changamoto ya kuukazia macho Msalaba wa Kristo, kielelezo cha upendo na mwaliko wa kujipatanisha na kumrudia Mungu, ili kupata amani na utulivu wa ndani!

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree