BREAKING NEWS

Thursday, 25 February 2016

Mtandao wa utume wa sala duniani!



atika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya habari, changamoto ambayo imevaliwa njuga na mtandao wa utume wa sala duniani, unaoendelea kusoma alama za nyakati, ili ujumbe na nia za Baba Mtakatifu kila mwezi ziweze kuwafikia watu wengi zaidi mahali walipo! Utume wa sala kwa sasa unaendelea kutumia mitandao ya kijamii, ili kuweza kuwashirikisha waamini wengi katika sala, huku wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu.
Kwa mwaka huu, Baba Mtakatifu anaendelea kutoa ujumbe wake kwa njia ya video na mwakani, yaani 2017, Baba Mtakatifu ataendelea kutoa tafakari za mara kwa mara kadiri atakavyoona kwa kusoma alama za nyakati. Haya yanafafanuliwa na Padre Frèdèric Fornos, Mkurugenzi mkuu wa Utume wa Sala duniani katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano. Mabadiliko yanayotekelezwa kwa wakati huu ni kutaka kukuza na kudumisha ari na mwamko wa umissionari wa Kanisa unaojikita katika mahusiano ya ana kwa ana na Kristo Yesu.
Utume wa sala ni mtandao wa sala unaowaunganisha waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia unaoratibiwa na Wayesuit, ili kumsindikiza Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake. Maboresho yanayoendelea kufanyika ni kuliwezesha Kanisa kutekeleza vyema dhamana na utume wake wa kimissionari. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaliwezesha hata Kanisa kuweza kuvuka mipaka ya kijiografia na kuwa karibu zaidi na watu kwa njia ya mitandao ya kijamii. Watu wanavutwa zaidi na ushuhuda ndiyo maana hatua ya kwanza imekuwa ni kuweka ujumbe wa Baba Mtakatifu katika video, ili watu waone na kushiriki pamoja naye katika sala, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa duniani. Lengo ni kukuza mahusiano kati ya mwamini na Baba Mtakatifu katika sala inayomwilishwa kwenye matendo!
Itakumbukwa kwamba, nia za Baba Mtakatifu zinaandaliwa walau miaka miwili kabla, kwa kuzingatia mahitaji ya Kanisa, ili hatimaye, kuweza kuzitafsiri katika lugha mbali mbali na hatimaye Papa mwenyewe kutoa ridhaa yake kwa nia hizi. Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha wadau wa utume wa Sala kusoma alama za nyakati. Kuanzia mwaka 2017 kutakuwa na nia maalum na tukio, litakalishirikisha Kanisa zima, ili kukabiliana vyema na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa. Nia za Baba Mtakatifu zinalenga kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya Wakristo, ufunguo makini katika utume wa Kanisa.
Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanahamasishwa kusali zaidi ili kufanikisha mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji. Kwa kutumia mitandao ya kijamii, Wakristo wengi wataendelea kuunganishwa, ili kuwawezesha kushiriki katika mchakato wa kuleta ari na mwamko mpya wa utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree