Thursday, 25 February 2016
Upendo ni kiini na asili ya maisha na utume wa Kanisa!
Posted by Unknown on 23:36:00 in | Comments : 0
Imekwishagota miaka 10 tangu Papa Mstaafu Benedikto XVI alipochapisha Waraka wa kitume “Mungu ni upendo” "Deus Caritas est"; waraka ambao kwa sasa ni kama mwongozo wa utekelezaji wa mchakato wa umwilishaji wa matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha ya Wakristo. Waraka wa Mungu ni upendo ni endelevu na kamwe hauwezi kupitwa na wakati kwani ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa.
Upendo unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, Kristo Yesu aliyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu; upendo ambao Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wana umwilisha katika uhalisia wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji!
“Upendo haupungui neno wakati wowote” ndiyo kauli mbiu inayoongoza Kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Kipapa linaloratibu Misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 26 Februari 2016 mjini Vatican. Hii ni fursa ya kutafakari kwa kina dhana ya upendo wa Mungu katika mwelekeo wa kitaalimungu na shughuli za kichungaji, hususan wakati huu Mama Kanisa anpoadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu. Kumbe, kongamano hili ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mungu ni upendo ni Waraka wa kwanza kabisa ulioandikwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI mara baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.
Monsinyo Giampietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum anasema, upendo wa Mungu ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa, mintarafu ufunuo wa Kristo uliojionesha kwa namna ya pekee kabisa katika maisha, maneno na matendo yake. Kanisa katika ulimwengu mamboleo linapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, Matendo ya huruma kiroho na kimwili ni mambo msingi katika mchakatowa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha.
Monsinyo Dal Toso anakaza kusema, upendo wa Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Hapa kuna haja ya kutofautisha kati ya upendo wa kibinadamu na upendo wa Kimungu. Upendo unaoshuhudiwa na Kanisa ni kielelezo cha Mungu mwenyewe kwani Mungu ni upendo kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kichungaji. Upendo wa kibinadamu unapata utimilifu wake katika upendo wa kimungu. Upendo huu unatafsiriwa kwa lugha ya Kigiriki kuwa ni Agape, kwa Kilatini, Caritas. Kanisa linapenda kukazia huduma ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wake. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa makini ya kutoa kipaumbele cha pekee katika upendo unaobubujika kutoka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kutambua kwamba, upendo wa Kimungu unalikamilisha na kuliwezesha Kanisa kusimama kwa miguu yake.
Monsinyo Dal Toso anafafanua kwamba, upendo wa Mungu unaliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake msingi, changamoto na mwaliko kwa Wakristo ambao ni viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha pekee kwa dhana ya upendo katika maisha yao. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wamwone na kuguswa na Kristo Yesu kwa njia ya upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha anasema Baba Mtakatifu Francisko.
Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI umekuwa kweli ni dira na mwongozo kwa wafanyakazi wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maskini, wakimbizi, wahamiaji, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Kuna mafanikio makubwa yanayojionesha, lakini kwa mtazamo wa kibinadamu, si rahisi kuweza kuyaona kwani upendo na kiini na asili ya Kanisa. Huduma ya upendo ni muhimu sana na kwamba, Waraka huu utaendelea bado kuwa ni changamoto kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa hususan katika huduma makini kwa maskini.
Ni waraka unaowachangamotishwa wafanyakazi na viongozi wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia ukweli na uwazi; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa linahamasishwa kushuhudia ujumbe endelevu wa Kristo kwamba, Mungu ni upendo ambao kwa namna ya pekee, umeshuhudiwa na Kristo Yesu!
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment