Polisi
nchini Burundi wamewakamata waandishi habari wawili raia wa Uingereza
na Ufaransa katika msako uliofanyika kuwasaka waasi katika mji mkuu,
Bujumbura.
Maafisa
wa usalama wametangaza Ijumaa kuwa waandishi habari hao ni Phil Moore wa
Uingereza na Jean Philippe Remy wa Ufaransa na kwamba wamekamatwa
katika msako uliofanyika katika mitaa ya Jabe na Nyakabiga jijini
Bujumbura. Naibu Msemaji wa Polisi ya Burundi Moise Nkurunziza amesema
mwandishi habari Mfaransa alikamatwa alipofika kituo cha polisi kuuliza
kuhusu hali ya mwenzake Muingereza aliyekuwa ameshakamatwa.(VICTOR)
Gazeti la
Le Monde la Ufaransa limetoa taarifa likitaka waandishi hao waachiliwe
na kusema walikuwa ni maripota wake maalumu nchini Burundi. Hayo
yanajiri masaa machache baada ya Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty
International (AI) kutangaza kuwa, picha za satalaiti zinaonyesha
uwezekano wa kuweko makaburi matano ya umati katika eneo la Buringa
kaskazini mwa mji mkuu wa Burundi, Bujumbura.
Machafuko
yaliikumba Burundi tangu mwezi Aprili mwaka uliopita baada ya Rais
Nkurunziza kuteuliwa na chama chake cha CNDD-FDD kuwania tena urais kwa
mara ya tatu. Wapinzani walisema suala hilo ni kinyume cha katiba ya
nchi na makubaliano ya amani ya Arusha. Takribani watu 400 wamepoteza
maisha katika machafuko hayo huku makumi ya maelfu ya wengine wakiwa
wakimbizi.CHANZO:IRB SWAHILI
Post a Comment