Imekwisha gota miaka 500 ya kinzani na mipasuko ya kidini kati ya Wakatoliki na Waluteri; lakini katika kipindi cha miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Waamini wa Kanisa Katoliki na Waluteri kwa kujikita katika umoja na udugu.
Kwa mara ya kwanza, Khalifa wa Mtakatifu Petro anashiriki katika maadhimisho ya Mageuzi makubwa ndani ya Kanisa yaliyofanywa kwa unyenyekevu, huku wote wakiomba toba na huruma ya Mungu, ili kuambata ya mbeleni kwa moyo wa upendo na mshikamano wa dhati, kama kielelezo cha ushuhuda wa umoja unaojikita katika Ubatizo na Imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa pamoja, Makanisa yanapania kuendeleza mchakato wa maboresho ya dhati kati ya Makanisa.
Askofu mkuu Brian Farrel anakaza kusema, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika kipindi cha miaka 50 iliyopita wamesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika: upendo, ukweli, sala na damu ya mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Majadiliano katika ukweli, yameyawezesha Makanisa kufafanua matatizo, changamoto na fursa katika masuala ya kitaalimungu.
Kumekuwepo na majadiliano ya upendo yanayojikita katika uhalisia wa maisha ya Wakristo, kwa kupokeana na kusaidiana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu. Lakini kumekuwepo pia na majadiliano ya damu inayoendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani kwa Kristo na Kanisa lake, mambo yote haya yanawasukuma Wakristo wa Makanisa mbali mbali kujikita katika mshikamano, umoja na upendo wa kidugu.
Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo limeendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, kwa kuona pia mchango mkubwa ulioletwa na Mageuzi ya Luteri ndani ya Kanisa. Waamini wengi kwa sasa wamekuwa na mwamko wa kutaka kusoma, kutafakari na kulifahamu Neno la Mungu, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, wakati ambapo Biblia ilibaki kuwa ni “mali ya wakleri” peke yao. Kumekuwepo na marekebisho makubwa katika maisha na utume wa Kanisa kadiri ya changamoto zilizotolewa na Luteri kwa wakati ule. Alitaka kuona Kanisa ambalo ni moja, takatifu na linalojikita katika ukweli na uwazi mchakato ambao ulianzishwa na Mtaguso wa Trento na baadaye Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwa sasa unaendelezwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa.
Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi makubwa ndani ya Kanisa yatawashirikisha viongozi wakuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani Mheshimiwa Martin Junge, Askofu Munib A. Younan. Kwa pamoja watatumia Kitabu cha Sala ya Pamoja “Common Prayer” kilichoandaliwa hivi karibuni kwa ajili ya maadhimisho haya.
Kwa upande wake Mheshimiwa Martin Junge anasema, maadhimisho haya yanajikita katika Uekumene unaowajibika, baada ya Makanisa haya mawili kujikita katika mchakato wa upatanisho, haki na amani; kwa sasa wanataka kushuhudia kwa pamoja tunu hizi msingi zikimwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa kwa imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Maadhimisho haya yatasaidia kuimarisha umoja wa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Lengo ni Wakristo katika umoja wao, wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, kwa kumshuhudia Kristo Yesu. Tamko la pamoja kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani lilifungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Makanisa haya mawili.
Post a Comment