WANANCHI wa Kijiji cha Kipuma,kata ya Ndulungu,wilayani Iramba
wamemhakikishia diwani wa kata hiyo kuwa pamoja na wilaya hiyo kukumbwa na
ugonjwa wa kipindupindu lakini wao bado wanaendelea na ukorogaji,uuzaji pamoja
na unywaji wa pombe za kienyeji.
Kauli hiyo imetolewa na wananchi wa Kijiji cha Kipuma,kata
ya Ndulungu kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika katika shule ya msingi Kipuma,kwa lengo la kusomewa
taarifa ya mapato na matumizi ya Kijiji hicho,ambayo hata hivyo haikuwezekana
kutokana na kutoandaliwa kikamilifu.
Wananchi hao wamesema wamelazimika kuendelea na hatua hiyo
kutokana na viongozi wao,hususani wenyeviti wa vitongoji kuwatoza shilingi
50,000/= na hivyo kuona kwamba upo uhalali wa wao kuendelea kukoroga,kuuza na
kunywa pombe hiyo ambayo inaweza kuhatarisha afya na maisha yao kwa ujumla.
Akifunga mkutano huo,diwani wa kata hiyo,Bwana Iddi Munyonga ametangaza
amri halali ya kupiga marufuku watu kukoroga,kuuza na kunywa pombe na kuonya
kwamba yeyote atakayepatikana akikiuka agizo hilo atakamatwa na kufikishwa
katika baraza la kata kwa hatua zaidi za kisheria.
Hata hivyo diwani huyo amefafanua kwamba sababu za serikali
wilayani humo kuzuia ukorogaji,uuzaji na unywaji wa pombe umetokana na kuwepo
kwa ugonjwa wa kipindupindu,na kwamba mpaka sasa wilaya ya Iramba ndiyo bado
inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa wa kipindupindu kati ya wilaya za Mkoa wa
Singida.
Kutokana na kuwepo kwa ugonjwa wa kipindupindu,Bwana Munyonga
amesema kumechangia minada kufungwa na kusababisha pia bei za mazao na hata
mifugo kushuka jambo linaloweza kushusha uchumi wa mtu mmoja
mmoja,kata,wilaya,mkoa na hata taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa diwani Munyonga ametumia fursa hiyo kuwakumbusha
wananchi hao juu ya umuhimu wa kujenga utamaduni wa kuweka mazingira yao katika
hali ya usafi na kuwaagiza wajumbe wa serikali ya Kijiji waanze kufanya ukaguzi
wa nyumba hadi nyumba kwa lengo la kuchukua tahadhari ya magonjwa ya mlipuko.
Hata hivyo mwakilishi huyo wa wananchi amebainisha kuwa kuna
taarifa kwamba idadi kubwa ya watu wanaochimba madini hawana vyoo hivyo upo
uwezekano mkubwa wa kukumbwa na magonjwa mbalimbali ya milipuko na hivyo
kuhatarisha afya na maisha yao kwa ujumla.
Post a Comment