BREAKING NEWS

Wednesday, 27 January 2016

Familia ya Mungu Ghana yakunja jamvi la Mwaka wa Watawa Duniani!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani unaohitimishwa rasmi hapo tarehe 2 Februari 2016 katika Maadhimisho ya Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa Duniani, aliwataka watawa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.
Familia ya Mungu nchini Ghana, imehitimisha maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, hapo tarehe 25 Januari 2016, kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani, sifa, utukufu na heshima, kuwateuwa watawa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya furaha na huruma ya Mungu kwa waja wake.  Katika maadhimisho haya, Familia ya Mungu nchini Ghana imejikita katika mambo makuu matatu yaliyowataka watawa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na utakatifu wa maisha.
Hili ni tukio ambalo limewakushanyisha Zaidi ya watawa mia tano kutoka katika Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yapatayo sitini yanayotekeleza dhamana na utume wao nchini Ghana. Watawa wanasema, changamoto zinazoikabili dunia na Kanisa katika ujumla wao, ni changamoto ambazo pia zinawakumba watawa katika maisha na utume wao, kumbe, wanapaswa kusimama kidete katika sala, maisha ya kijumuiya, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda amini unaofumbatwa katika kanuni, utume na roho za mashirika yao, tayari kuwamegea watu wa Mungu huruma na upendo wa Kristo unaofumbatwa katika huduma mbali mbali za maisha ya kiroho na kimwili zinazotekelezwa na watawa nchini Ghana.
Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, watawa wamewamegea na kuwashirikisha Watu wa Mungu: huruma, upendo na urafiki unaofumbatwa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Watawa ni mashuhuda na “majembe” makini ya upendo wa Mungu unaomwilishwa katika ushuhuda wa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu kwa waja wake. Maadhimisho haya yamehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa nchini Ghana.
Watawa wametakiwa kukuza na kudumisha malezi ya awali na endelevu; kwa kujikita katika tafakari, sala, maisha ya kijumuiya na Sakramenti za Kanisa, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Watawa wawe na msingi thabiti wa maisha ya kiroho, kiutu, kisaikolojia, kiakili na kijamii, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu, Kanisa linapoadhimisha pia Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Watawa wawe waaminifu kwa nadhiri, sharia na kanuni za maisha ya kitawa.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree