Wednesday, 27 January 2016
Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na wala si haki ya wazazi!
Posted by Unknown on 09:01:00 in | Comments : 0
Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Kamati kuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumatatu, tarehe 25 Januari 2016 amegusia kuhusu utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho ambao Kanisa Katoliki nchini Italia limeupata wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Kitaifa Jimbo kuu la Firenze; Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; mshikamano wa dhati kati ya viongozi wa Kanisa na Jamii inayowazunguka; umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao Barani Ulaya.
Kardinali Bagnasco anakaza kusema, Kongamano la Kijamii Jimbo kuu la Firenze lilijikita katika dhana ya Sinodi, changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kuamua na kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji katika umoja na mshikamano. Lengo ni kukuza na kuendeleza ari na mwamko wa kimissionari, ili kuwatangazia watu wa Mataifa Injili ya huruma ya Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha.
Kardinali Bagnasco anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki linaendelea kukazia umuhimu wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika sera na mikakati yake ya kichungaji, ili kuwawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutangaza na kushuhudia Injili ya familia ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto nyingi. Umoja na udumifu wa familia; malezi na matunzo bora ya watoto ni kati ya mambo msingi yanayopaswa kudumisha ndani ya familia, ili kuiwezesha familia kuwa ni kitovu cha Uinjilishaji mpya unaojikita zaidi katika ushuhuda wa imani tendaji.
Maaskofu Katoliki Italia wanaendelea kuhimiza umuhimu wa shule kama sehemu muhimu sana ya majiundo ya mtu kijamii. Hapa vijana wa kizazi kipya hawana budi kufundwa na kupewa elimu inayogusa majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, Kanisa kwa kuchota katika utajiri wake kwenye sekta ya elimu linapania kushirikisha utajiri huu katika majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya ili kujikita katika mambo msingi ya maisha.
Maaskofu wanakumbusha kwamba, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kiini na walengwa wa Habari Njema ya Wokovu, wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa Katoliki nchini Italia litaendelea kuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahumia maskini wa hali na mali, ili kudumisha utu na heshima yao kama binadamu.
Kardinali Bagnasco anasema, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yawasaidie waamini kujenga na kudumisha: imani, matumaini, mapendo, haki na amani, kwa kujibu kikamilifu mahitaji ya binadamu wa nyakati hizi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wajenge na kukoleza moyo wa ukarimu, umoja na mshikamano, tayari kupitia kwenye Lango la huruma ya Mungu, ili kuonja uwepo endelevu wa Mungu katika maisha ya watu wake. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa makini ya toba, wongofu wa ndani, upyaisho wa maisha ya kiroho, ukuaji wa Kanisa na mwendelezo wa mchakato wa Uinjilishaji mpta unaojikita katika ushuhuda wa maisha.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawaalika viongozi wa Kanisa kuwa karibu zaidi na watu wao: kiroho na kimwili, ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana; athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; ili kuwaonjesha huruma na mshikamano katika hija ya maisha yao ya kila siku. Bado kuna watu zaidi ya millioni nne wanaoishi katika umaskini wa hali na kipato nchini Italia. Kanisa kwa namna ya pekee, limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia na kuwwasaidia watu wanaoogelea katika dimbwi la umaskini kwa kuwapatia chakula na malazi.
Kwa namna ya pekee, Kardinali Bagnasco umekazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kutambua haki na wajibu wake. Familia inajengwa katika mahusiano thabiti kati ya bwana na bibi na matunda ya muungano huu wa upendo ni watoto ambazo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si haki ya wazazi; wanapaswa kupokelewa na kutunzwa kwa heshima na nidhamu. Watoto wanayo haki msingi ya kukua na kulelewa na baba na mama, hitaji msingi la kibinadamu la wala si sera ya kisiasa.
Kuhusu tunu msingi za maisha ya Ndoa na Familia, Kanisa Katoliki nchini Italia limeshikamana na kufungamana, ili kuziwezesha familia kuwa kweli ni watangazaji na mashuhuda wa Injili ya familia. Waamini walei pamoja na watu wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Kanisa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasikitika kusema kwamba, wakimbizi na wahamiaji wengi wanaendelea kukumbana na maafa kutokana na utamaduni na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani; utamaduni ambao unaangalia zaidi mafao ya kisiasa kuliko utu na heshima ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu kwa kujikita katika sera za kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Huu ni wajibu na dhamana ya wadau mbali mbali, ili kuwaonesha watu hawa uso wa huruma ya Mungu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment