BREAKING NEWS

Thursday, 21 April 2016

Waziri Mkuu Aongoza Wakazi Wa Dodoma Mazishi Ya Askofu Isuja wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya waumini na wakazi wa mkoa wa Dodoma katika mazishi ya Mhashamu Askofu Mstaafu, Mathias Isuja wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma.

Amesema kifo hicho ni pigo kwa watu wote na si kwa kanisa pekee kwa sababu walimtegemea kulisaidia Taifa kiroho na kimaendeleo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 20, 2016) wakati akizungumza na waumini na wakazi wa mkoa huo na mikoa jirani kwenye ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiaskofu la Mtume Paulo wa Msalaba mjini Dodoma.

Askofu Isuja ambaye alizaliwa Agosti 14, 1929 alikuwa Askofu wa kwanza mzalendo katika Jimbo la Kanisa Katoliki la Dodoma. Alistaafu kazi ya uaskofu mwaka 2004 kwa mujibu wa sheria ya kanisa. Alifariki Aprili 13, mwaka huu.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kumuenzi Askofu Isuja kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa uhai wake na kuyaendeleza yote aliyoyaanzisha kwenye maeneo aliyowahi kuyatumikia.

“Tumepoteza mtu makini, sisi ni mashahidi wa mchango mkubwa wa marehemu siyo tu katika kutoa huduma za kiroho, bali pia huduma za kijamii zilizolenga kuleta maendeleo kwa wananchi katika jimbo hili la Dodoma na katika taifa kwa ujumla,” amesema.

Mapema, akitoa mahubiri wakati wa ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Judathadeus Ruwa’ichi alisema waumini wa kanisa hilo wa mkoa wa Dodoma na Tanzania nzima wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha marefu aliyomjalia Askofu Isuja.

“Tunapaswa kumshukuru kwa maisha marefu ambayo Mungu alimzawadia baba yetu Isuja. Katika Zaburi ya 90 tunasoma kuwa mwanadamu ana miaka ya matazamio ambayo ni 70, lakini yeye alipewa miaka ya matazamio 70 na akazawadiwa nyongeza ya miaka 10 na kisha miaka mingine sita na nusu,” alisema.

Alisema zawadi nyigine ambayo Mungu aliwapatia waumini hao ni ya imani ambayo Baba Askofu Isuja aliipokea, aliifundisha na aliishi na akawataka waendelee kumshukuru Mungu kwa hilo.

“Miaka 56 ya utumishi wake kama padre na askofu ni zawadi kwa Dodoma na Tanzania na siyo kwake yeye binafsi,” alisema.

Ibada hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na Maaskofu Wakuu na Maaskofu wa kawaida 28 kutoka majimbo ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Njombe, Mpanda, Iringa, Songea, Tabora, Morogoro na Mahenge. 

Mengine ni Musoma, Rulenge, Mbinga, Moshi, Same, Kahama, Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara na Lindi. Majimbo mengine ni Bukoba, Tanga, Singida, Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Kondoa na Kayanga.
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980.
DODOMA.

JUMATANO, APRILI 20, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mathias Isuja  katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa  Kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba,  Aprili  20, 2016.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mathias Isuja katika mazishi yaliyofanyika kwenye Kanisa   Kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba Aprili 20, 2016.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree