BREAKING NEWS

Thursday, 7 April 2016

Viongozi CUF washutumiwa kwa kukosa uzalendo


Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekishiutumu Chama cha Wananchi (Cuf) pamoja na viongozi wao kwa kukosa uzalendo kutokana na kauli zao za kuunga mkono wahisani kuisitishia misaada Tanzania.

Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa kuteuliwa kutoka katika chama cha Ada-Tadea, Juma Ali Khatib ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa marudio, alipokuwa akichangia hotuba ya Rais wa Zanzibar kwenye baraza hilo mjini hapa.

Alisema, viongozi wa Cuf wameonesha udhaifu mkubwa wa kukosa uzalendo kwa kitendo chao cha kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kususa misaada kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema, Zanzibar ni nchi yenye kufuata katiba yake kwa hiyo ilikuwa na mamlaka kamili kupitia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kuitisha uchaguzi wa marudio baada ya kuufuta wa Oktoba 25, mwaka jana.

“Nimesikitishwa na kauli za viongozi wa Cuf kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kuhusu uamuzi wa kususia misaada kwa Tanzania. Viongozi hao wameonesha udhaifu na kukosa uzalendo,” alisema Khatib.

Alisema chama chake kiliamua kuingia katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20 kwa sababu umeitishwa na chombo halali kwa mujibu wa katiba, chenye majukumu ya kusimamia uchaguzi kikiwa hakiingiliwi na mtu yeyote.

Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini , Machano Othman Said, alisema kitendo cha viongozi wa Cuf kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kususa kutoa misaada kwa Tanzania hakikubaliki hata kidogo kikionesha udhaifu mkubwa wa viongozi hao katika uzalendo wa nchi.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree