Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka amesema yupo
tayari kulipa kodi ya mapato ya Sh586 milioni iwapo Mahakama itaamuru
hivyo.
Kodi hiyo inatokana na Sh1.617 bilioni alizopewa na
mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemalira ambazo zilidaiwa kuchotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Profesa Tibaijuka
aliyasema hayo jana baada ya taarifa kwamba Bodi ya Rufani ya Kodi
Tanzania (TRAB), imeagiza utekelezaji wa suala hilo ili kutimiza matakwa
ya sheria kuhusu mapato nchini.
“Ni kweli ninadaiwa kodi ya
Sh586 milioni, ila nimeenda mahakamani kutaka ufafanuzi kama ni halali
kufanya hivyo kwa fedha zilizotokana na mchango,” alisema Profesa
Tibaijuka na kuongeza “Nilipewa fedha kwa ajili ya shule lakini nadaiwa
kama ni kipato binafsi, hivyo nataka Mahakama iseme, ikikubali nitalipa
bila shida yoyote.”
Mbunge huyo alifafanua kuwa, anatambua
kulipa kodi ni suala la kila mwananchi na anachotaka ni ufafanuzi wa
uhusiano uliopo kati ya mapato na kodi.
Alisema lengo ni kutaka
kujua iwapo mchango ni sehemu ya fedha zinazostahili kutozwa kodi, bila
kujali zimepokelewa zikiwa taslimu au kupitia kwenye akaunti benki.
“Nipo
msibani hivi sasa. Watu wanakuja kunipa pole, wengine wanatoka Dar na
wasioweza wanatuma michango yao na hapa ndipo nisipoelewa dhana ya kodi
kwenye michango. Hii nayo inastahili kuingizwa kwenye mkumbo huo?”
alihoji.
Msemaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard
Kayombo alithibitisha kutolewa kwa hukumu hiyo kwenye pingamizi la
makadirio aliloliweka mbunge huyo na kueleza kuwa bado anaweza akatafuta
haki kwenye mamlaka za juu kama hajaridhika.
“Shauri lake liliamriwa Machi 29 na akatakiwa kulipa kiwango hicho alichokadiriwa,” alisema.
Mbunge
huyo wa Muleba Kusini, alitakiwa kulipa fedha hizo baada ya TRAB
kutupilia mbali rufaa yake ya kupinga kulipa zaidi ya Sh500 milioni.
Profesa
Tibaijuka, Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
alikata rufaa hiyo baada ya TRA kumtaka alipe kodi ya mapato
Sh586,364,625 kutokana na fedha alizopokea kutoka kwa Mkurugenzi wa
Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, Rugemalira.
Profesa
Tibaijuka ambaye alipokea fedha hizo kupitia akaunti yake iliyopo Benki
ya Mkombozi, zilisababisha kuvuliwa uwaziri na Rais mstaafu, Jakaya
Kikwete.
Alisema fedha hizo hazikuwa zake binafsi bali zilitolewa msaada kwa Taasisi ya Joha Trust.
Hata
hivyo, TRA kupitia kwa Wakili wake, Noah Tito ilisema Tibaijuka
anawajibika kulipa kodi hiyo kwani fedha hizo ziliingia katika akaunti
yake binafsi.
Post a Comment