Mbunge
wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amekanusha taarifa zilizosambaa katika
mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari kuwa yeye ni mmoja wa
wamiliki wa kampuni ya Lugumi, inayodaiwa kupewa zabuni ya kufunga
mashine za kuchukua alama za vidole kwenye vituo vya Polisi.
Ridhiwani
ametajwa katika habari hizo kuwa ni mmiliki wa kampuni ya Lugumi pamoja
na wamiliki wengine ambao ni Said Lugumi na aliyekuwa mkuu wa Jeshi la
Polisi, Said Mwema.
Ridhiwani
ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema
yeye hahusiki na kampuni yoyote ya Lugumi ingawa wana urafiki wa
kawaida na mmiliki wa kampuni hiyo.
“Kwanza
kabisa mimi si mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, hilo ni jambo la
msingi kabisa watu waelewe na sijawahi kufanya biashara yoyote na
Lugumi. Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo tunafahamiana naye
na ni rafiki yangu,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani
alisisitiza kuwa hana uhusiano wa kibiashara na mtu huyo na kwamba
hafahamu ni kwa nini amehusishwa na kampuni ya Lugumi.
“Hapa
ni watu tu wanaamua kuingiza tu maneno yao, haya maghorofa ninayotajwa
kumiliki Dar es Salaam hata sijawahi kutembelea ujenzi wake, wameamua
kuniingiza, Lugumi nafahamiana naye binafsi tu lakini wananiingiza,” alisema Ridhiwani.
Alisema
jambo hilo bado liko ndani ya Kamati ya Bunge na baadae ameliona kwenye
magazeti ya juzi kuwa Jeshi la Polisi litatoa taarifa yao, hivyo
asingependa kulizungumzia kwa undani.
Hivi
karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilitoa
siku saba kwa Jeshi la Polisi nchini kupeleka mkataba walioingia baina
yao na Kampuni ya Lugumi.
Kamati
hiyo ilipokutana na Jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka
2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly alisema jeshi
hilo mwaka 2011 liliingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya kufunga
mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya Polisi vya wilaya
nchi nzima ambavyo viko 108.
Alisema
mkataba huo ulikuwa wa Sh bilioni 37 pamoja na kodi na kwamba hadi sasa
kampuni hiyo imeshapewa asilimia 99 ya fedha zote ili hali vituo
vilivyofungwa mashine hizo ni 14 tu, kati ya vituo vyote 108.
Ridhiwani
alisema angependa jamii ifahamu kuwa hana uhusiano na kampuni hiyo kwa
kuwa hafahamu kabisa hata malipo yaliyofanywa kati ya Serikali na
kampuni ya Lugumi anasikia tu kama ambavyo watu wengine wamesikia.
Post a Comment