Mwenyekiti
wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) taifa, Augustine Mrema amemuunga
mkono Rais John Mgufuli kwa kasi yake ya kupambana na ufisadi na
kumuomba ampe kazi ili amsaidie kutekeleza jukumu hilo.
Mrema
alimuomba Rais Magufuli atambue uzoefu wake kwa kukumbuka jinsi
alivyopambana na mafisadi wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu
Waziri Mkuu.
Huku
akieleza CV yake hiyo, Mrema alimkumbusha Rais kuhusu ahadi aliyompa
wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, ya kumpa kazi
katika Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa atashinda na kuwa Rais.
Akizungumza
na waandishi wa habari kijijini kwake Kiraracha mkoani Kilimanjaro,
Mrema alisema kuwa anasikitishwa na ukimya wa Rais Magufuli kwa sababu
aliamini kuwa angetekeleza ahadi hiyo ya kumpa kazi muda mfupi baada ya
kutangaza Baraza la Mawaziri, jambo ambalo hadi sasa hajalifanya.
Alisema,
alikutana na Rais Magufuli mwaka jana katika kampeni jimboni Vunjo
kwenye eneo la Njia Panda lililopo ndani ya mji mdogo wa Himo na
kuambatana naye kwenye mkutano wa hadhara, ambapo alimwombea kura kwa
wafuasi wake na kuahidiwa ajira.
“Katika
kampeni, Dk Magufuli alifika kwenye mkutano wangu nikamwombea kura kwa
kuwaambia watu wangu wamchague kwa kuwa ni mchapakazi na mwadilifu.
Aliahidi kunipatia kazi katika Serikali na sasa namkumbusha na kumuuliza
mbona yupo kimya?” Mrema alieleza na kuhoji.
Alipoulizwa
ni kazi gani inayomfaa katika Serikali ya Magufuli, alisema yeye
alishawahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu hivyo yuko
tayari kufanya kazi yoyote itakayomfaa ila alitamani zaidi kupangwa
sehemu nyeti ili amsaidie kutumbua majipu.
Mrema
alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada binafsi za kutumbua majipu
anazozifanya na alijigamba kuwa yeye ndio mwenye uzoefu wa kupambana na
mafisadi kutokana na rekodi yake nzuri ya kipindi cha Rais wa Awamu ya
Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Katika
hatua nyingine, Mrema alikanusha taarifa ya kuhongwa fedha ili kufuta
kesi ya kupinga matokeo aliyoifungua dhidi ya Mbunge wa jimbo hilo,
James Mbatia.
Alisema, taarifa hizo ni za kupuuzwa kwa sababu zinalenga kumpaka matope kwa wananchi wake wa Vunjo.
Mrema
alieleza kuwa walifikia maridhiano ya pamoja kuhusu kuondoa kesi hiyo
mahakamani na kwamba, hilo lilifanywa kwa kuzingatia maslahi ya
wananchi.
Pamoja
na hayo, alikiri kumlipa Mbatia Sh mil 40 ikiwa ni sehemu ya kupunguza
gharama alizotumia katika kesi hiyo, ikiwemo malipo ya mawakili wake.
Post a Comment