Baada ya TAKUKURU kumpandisha
mahakamani wiki iliyopita kwa kuomba rushwa ya milioni 30, shirika la
Viwango Tanzania (TBS) nalo limeifunga Bekari yake( tanuri mikate ) kwa muda usiojulikana kwa kutotimiza masharti ya viwango vya ubora.
Tanuri
mikate hiyo pamoja na zingine 3 za watu wengine zilizopo Mkoani
Morogoro, zilikaguliwa kwa mara ya kwanza Julai mwaka jana na wamiliki
wake kupewa muda wa miezi sita kurekebisha kasoro zilizokuwepo, lakini
hadi Machi 10, mwaka huu katika ukaguzi mwingine walikuwa hawajatekeleza
na kutimiza masharti yaliyotolewa na TBS.
Mkaguzi
wa TBS, Ashura Katunzi alisema kazi ya kuzifungia tanuri mikate hizo
ipo kisheria baada ya wamiliki wake kushindwa kufuata utaratibu
walioelekezwa awali wa kurekebisha kasoro kabla ya kuanza kwa uzalishaji
tena.
Katunzi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Ubora wa TBS, alisema: “Kabla
ya kufunga bekari hizi, wakaguzi wa TBS walizitembelea tena mnamo Machi
10, mwaka huu ili kujiridhisha na iwapo utekelezaji umefanyika katika
kipindi cha miezi sita waliopewa, lakini hakuna kilichofanyika,” alisema Katunzi juzi wakati wakifanya ukaguzi na kuchukua uamuzi huo.
Alisema
kutokana na kukaidi agizo hilo, TBS imezifungua kwa muda usiojulikana
hadi watakaporekebisha kulingana na maelekezo na kuomba upya kufunguliwa
baada ya ukaguzi mwingine kufanyika.
Tanuri
mikate zilizofungiwa kuanzia juzi ni MS Bakery Magooma Super Market
inayomilikiwa na Murad, Baraka Bakery mali ya Salim Nassor, Sifasita
Bakery inayomilikiwa na Tanzua Tambi na M&M Bakery mali ya Sarah
Sanya.
“Bekari
hizi zimekutwa zinafanya kazi katika mazingira hatarishi yasiyo salama
na yanatia hofu kwa mlaji, zina ukosefu wa vyoo, zipo kwenye makazi ya
watu na ukosefu wa vyumba vya kubadilisha nguo kwa wafanyakazi,” alifafanua Katunzi na kuongeza:
“Katika
ukaguzi wetu tumeona bekari hizi zina ukosefu wa eneo maalumu la
kuoshea vyombo, uchakavu wa sakafu, mikate kuwekwa sakafuni na ufinyu wa
eneo la kazi.”
Alisema
endapo wamiliki hao watarekebisha kasoro na kutimiza viwango vya ubora,
wanatakiwa kuwasilisha tena maombi rasmi TBS ili wakaguliwe tena ili
kujiridhisha iwapo wametimiza vigezo kabla ya kufunguliwa tena.
“Watakapoharakisha kufanya marekebisho waliyoelelezwa, ndipo watakapoweza kufunguliwa haraka kuendelea na uzalishaji tena,” alifafanua mkaguzi huyo wa shirika la viwango.
Naye
Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile alisema licha ya kuzifungia
tanuri mikate hizo, kazi hiyo inaendelea ili kuzifikia nyingine
zilizokaguliwa na kushindwa kutekeleza masharti yake.
Hivyo
alitoa mwito kwa wazalishaji wa mikate katika Manispaa ya Morogoro na
maeneo mengine wafuate utaratibu na kuweka ubora wa mikate kwa
kuzingatia viwango vya TBS kabla ya kufikisha sokoni kwa walaji.
Baadhi
ya wafanyakazi waliokutwa katika tanuri mikate hizo waliwasihi wakaguzi
wa TBS wasiwafungie na badala yake wawapatie muda wa ziada ili
warekebishe kasoro hizo wakati wakiendelea na uzalishaji, maombi
yaliyogonga mwamba kutokana na kufungwa kwa milango kwa makomeo chini ya
ulinzi wa Polisi.
Post a Comment