Rais
John Magufuli anataraji kusafiri tena kwenda nje ya nchi hivi karibuni
akiwa na msafara ambao unawezekana usizidi jumla ya watu 10.
Ilimchukua
Rais Magufuli siku 153 tangu kuapishwa kwake kufanya ziara ya kwanza ya
nje ya nchi baada ya kwenda Rwanda kwa mwaliko wa Rais Paul Kagame
Jumanne iliyopita.
Rais alikwenda Rwanda kwa ajili ya kufungua
daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha biashara chenye huduma za
pamoja, ambacho ni kiunganishi muhimu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika
safari hiyo, katika kile kinachoonekana kuwa ni muendelezo wa hatua
yake ya kubana matumizi ya serikali kadri iwezekanavyo, Rais Magufuli
alikuwa na msafara usiozidi watu 10.
Waziri wa Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa,
Balozi Augustino Mahiga, alisema jana kuwa Rais Magufuli anatarajia
kusaifiri tena kwenda nje ya nchi hivi karibuni.
Balozi Mahiga
alisema katika safari hiyo, msafara wake utaendelea kuhusisha watu
wachache wenye umuhimu katika safari husika ili kuepukana na gharama
zisizokuwa za lazima.
Hata hivyo, Balozi hakutaja nchi hiyo itakayofuatia baada ya ziara ya Rwanda wala siku ya kusafiri.
“Rais atasafiri tena hivi karibuni… na utaratibu huu wa kuwa na msafara wa watu wachache hautabadilika,” alisema Balozi Maiga.
Akiwa Rwanda, Rais Magufuli alisema hapendi kusafiri kwenda ughaibuni kwa sababu anapenda kubana matumizi kwa vitendo.
Akizungumzia
kauli hiyo, Mahiga alisema ni kweli, mara zote Rais Magufuli amekuwa
akisisitiza juu ya umuhimu wa kila mmoja ndani ya serikali yake kubana
matumizi yasiyokuwa ya lazima na ndiyo maana amekuwa akilidhihirisha
hilo kwa vitendo.
“Rais anachosema kuhusu kubana matumizi ni
kweli kabisa… ndiyo maana msafara wake katika ziara hiyo (ya Rwanda)
hatukuzidi watu kumi. "Hii inamaanisha hataki kuwapo kwa matumizi
makubwa katika safari za nje.”
Aidha, Balozi Mahiga alifafanua
kuwa baadhi ya mawaziri na maafisa wengine kadhaa walioshiriki shughuli
ya uzinduzi wa daraja la Rusumo waliishia hapo na kurudi wakati yeye na
maafisa wachache wa serikali wakiongozana na Rais katika ziara ya
Rwanda.
“Nafikiri mliwaona baadhi ya mawaziri pale Rusumo… wale
walitokea huku Tanzania na kurudi. Hawakuwamo katika msafara uliokuwa
Rwanda,” alisema Balozi Mahiga.
Post a Comment