BREAKING NEWS

Wednesday, 16 March 2016

Waziri Mwakyembe Akutana na Jaji Joseph Warioba Ili Kupata Maoni yake kuhusu Mahakama ya Mafisadi Nchini

 
Jaji Mstaafu Joseph Warioba amesema uamuzi wa serikali ya awamu ya tano wa kuanzisha mahakama itakayoshughulikia ufisadi, rushwa na uhujumu uchumi umekuja wakati muafaka lakini amependekeza kuwa mahakama pekee haiwezi kushughulikia suala hilo bila kushirikiana na Jeshi la Polisi na Takukuru.
 
Jaji Warioba amesema hayo leo wakati alipoalikwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusiana na serikali kuanzisha mahakama itakayoshughulikia Rushwa na wahujumu  uchumi.
 
“Mahakama pekee haiwezi kushughulikia ufisadi na uhujumu uchumi bila kushirikisha vyombo vingine ambavyo ni Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika kuimarisha mahakama hiyo ambayo inatarajia kuanzishwa hivi karibuni” amesema Jaji Warioba.
 
Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha  utaratibu wa kukutana na viongozi wa zamani ambao walishawahi kuongoza wizara hiyo kwa lengo la kupata mapendekezo, maoni na uzoefu juu ya kuanzishwa kwa mahakama. 

“Leo nimekaribishwa wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusiana na uanzishwaji wa mahakama itakayoshughulikia ufisadi, rushwa na wale wanao hujumu uchumi, huu ni uamuzi mzuri na hizi ni jitihada za wazi za serikali katika kupambana na rushwa”amesema Jaji Warioba.
 
Amesema lengo la serikali la kuanzisha kwa mahakama hiyo ni kupambana na ufisadi na tayari serikali ya awamu ya tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kuzuia mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Sheria na Katiba , Dk Harrison Mwakyembe amesema katika kipindi kifupi cha uongozi wa rais Magufuli masuala yote ya msingi aliyoyasema wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana ameshaanza kuyatekeleza.
 
“Uanzishwaji wa mahakama itakayoshughulikia ufisadi na uhujumu uchumi ni miongoni mwa vipaumbele alivyovitoa rais Magufuli wakati wa kampeni hivyo kwa kiasi kikubwa yale yote ambayo aliahidi kipindi cha uchaguzi ameanza kuyatekeleza”amesema Dk Mwakyembe.
 
Amesema mbali na uanzishwaji wa mahakama hiyo, pia suala la katiba mpya litashughulikiwa lakini kwa kuanza rais Magufuli ameanza na kuwawajibisha wale wote ambao wamekiuka maadili ya kazi zao pamoja na kuanzisha mahakama itakayoshughulikia ufisadi na uhujumu uchumi.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree