Takukuru imeanza kuchunguza taarifa kwamba Waziri wa Ardhi, William
Lukuvi alikataa kupokea rushwa ya Sh5 bilioni iliyotaka kutolewa na
wafanyabiashara wawili wakubwa ili kuwapitishia mradi wa Sh84 bilioni.
Katika mahojiano na gazeti la Mwananchi hivi karibuni, Waziri
Lukuvi alisema kwamba lengo la
wafanyabiashara hao ilikuwa ni kufanikisha mpango wao wa kuiuzia
Serikali ardhi kwa bei kubwa kwenye eneo linalotakiwa kujengwa mji wa
kisasa wa Kigamboni.
Licha ya kukataa kutaja majina ya
wafanyabiashara hao, Lukuvi alisema mtandao huo wa wafanyabiashara ni
hatari na unaweza kusababisha mtu ashindwe kufanya kazi ya wananchi
iwapo ataendekeza rushwa.
Jana, Mkurugenzi wa taasisi hiyo,
Valentino Mlowola alisema kutokana na taarifa ya kiongozi huyo, ofisi
yake iliamua kuchukua chanzo hicho na kuanza kazi ya uchunguzi.
Hata
hivyo, Mlowola hakutaka kuweka wazi kazi ya uchunguzi huo imeanza lini
wala ilipofikia.
“Kueleza tumeanza lini hilo ni suala la kiufundi,
tumeshaanza kushughulikia,” alisema Mlowola ambaye Rais John Magufuli
amemuidhinisha rasmi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo baada ya
kukaimu kwa miezi kadhaa.
Katika ufafanuzi wake, kamishna huyo
wa zamani na mkurugenzi wa Intelijensia ya Makosa ya Jinai katika Jeshi
la Polisi, alisema taasisi hiyo kwa sasa imekuwa ikichukua tuhuma yoyote
ya rushwa kutoka chanzo chochote baada ya kuripotiwa.
Katika
mahojiano hayo, Waziri Lukuvi alisema wafanyabiashara
hao waliwaeleza marafiki zake wa karibu kuwa wangempa rushwa.
Mji
huo mpya wa Kigamboni unajumuisha kata za Kigamboni, Tungi, Vijibweni,
Mjimwema, Kibada, Somangila na eneo lote hilo lina ukubwa wa takribani
ekari 6,000.
Awali mradi huo ulitarajiwa kugharimu Sh13 trilioni
ambazo zingetolewa na Serikali, lakini ikaamua kushirikisha sekta
binafsi ili kuujenga na Serikali ishughulikie uwezeshaji wa awali.
Lukuvi
ambaye alihamishiwa Wizara ya Ardhi mapema mwaka jana na kubakizwa
katika wizara hiyo na Rais Magufuli, alisema amegundua kuna mtandao
mkubwa wa rushwa unaoanzia ngazi ya halmashauri mpaka wizarani ambao
unahusisha maofisa wa Serikali na viongozi wa wizara.
“Kama
ukiwa na tamaa huwezi fanya kazi uliyotumwa. Kuna wakati walikuja ni
wafanyabiashara wawili wakubwa na kutaka wanipe Sh5 bilioni ili nikubali
kupitisha mradi wao wa mabilioni ya shilingi na walitangaza kwa
marafiki zangu kuwa wangenipa fedha, lakini hapa hawawezi,” alisema
Lukuvi.
Aliongeza: “Wakati naingia tu wizara hii nilikuta
harakati za kukamilisha mradi wa Kigamboni ukiwa katika hatua za mwisho
na kila kitu kilikuwa kimekamilika. Lakini nilipopitia vizuri nilikataa
kuwalipa wafanyabiashara hao. Cha ajabu hazikupita siku mbili walipata
taarifa wakaja mbio kutaka kuniona.”
Kwa mujibu wa Waziri
Lukuvi, wafanyabiashara hao walitaka walipwe Sh141 milioni kwa kila
ekari wakati wao walinunua ardhi kutoka kwa wananchi kwa Sh5 milioni kwa
ekari, jambo ambalo alisema lilishapitishwa awali.
“Niligundua
pale kuna udanganyifu na wizi mkubwa. Haiwezekani mwekezaji anunue
kutoka kwa wananchi ekari moja kwa Sh5 milioni, kisha Serikali tumlipe
Sh141 milioni kwa ekari kwa kuvuka pantoni tu. Ni wizi mkubwa.
"Kama kweli Serikali ina fedha hizo kwa nini tusimlipe mwananchi moja kwa moja?” alihoji.
Waziri
Lukuvi alisema endapo njama hizo zingefanikiwa, Serikali ingetumia
zaidi ya Sh84 bilioni kuwalipa wawekezaji hao hewa kwa kuwa mmoja
anamiliki takribani ekari 200 na mwingine 400.
“Niliwaambia
Serikali haiwezi kuwalipa fedha hizo na badala yake waende kuiendeleza
ardhi wenyewe kulingana na mradi unavyotaka. Walitaka kutajirika kwa
ujanja ujanja,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Eti walidai
wamekopa fedha benki kwa ajili ya mradi huo. Haiingii akilini mtu
utumie Sh5 milioni, halafu uje uvune mabilioni ya fedha kwa kuvuka
pantoni tu.”
Post a Comment