BREAKING NEWS

Wednesday, 2 March 2016

Sudani Kusini Yakubaliwa Kuwa Mwanachama Mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.....Liberate Mfumukeko Ateuliwa Kuwa Katibu Mkuu Mpya wa Jumuiya Hiyo



 Wakuu wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameikubalia Sudan Kusini kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.

Mkutano wa kilele wa Jumuiya hiyo jijini Arusha leo  Jumatano (Machi 2) umepitisha  pendekezo la baraza la mawaziri juu ya uwanachama wa Sudan Kusini na pia hali ya usalama nchini Burundi.

Kikao hicho kilichodumu kwa muda wa takribani masaa matano kimelikubalia taifa hilo changa kabisa barani Afrika kuwa mwanachama wake wa sita, kuungana na Tanzania, Rwanda, Burundi , Uganda na Kenya.

Rais  Magufuli  ambaye ndiye  mwenyekiti wa kikao hicho, amewaambia wajumbe wa mkutano huo wa kilele kwamba sasa "Sudan ya Kusini ni mwanachama halali wa jumuiya" hiyo.

Mkutano huo pia umezungumzia kwa kina masuala ya maendeleo ndani ya jumuiya ikiwemo mipango ya kujengwa kwa viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi ili kuondoa kabisa biashara ya uagizaji wa nguo kuukuu, maarufu kama mitumba, katika nchi hizo katika miaka michachache ijayo

Mkutano huo pia umeshuhudia uzinduzi wa pasi ya kusafiria ya kielektroniki itakayotumiwa katika eneo la Afrika Mashariki pamoja na mwongozo maalum wa kimaaadili katika biashara kwenye nchi wanachama wa jumiya hiyo.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya jumuiya hiyo, Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Dk. Richard Sezibera, amesema kuwa jumiya hiyo inasonga mbele kwani itifaki mbalimbali zimepitishwa kuanzia ushirikiano katika soko la pamoja, ushuru wa forodha na sasa wanaelekea kufikia hatua ya Afrika Mashariki kuwa na sarafu moja itakayotumika katika nchi zote wanachama.

Amesema kuwa tayari jitihada zinaendelea katika kuondoa vikwazo mbalimbali katika sekta za mawasiliano, biashara na usafiri "ili kuwapa wananchi wa Afrika Mashariki fursa ya kuufurahia na kufaidi muungano" huo.

Katika mkutano huo, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi hakuhudhuria na badala yake alimtuma makamu wake wa pili, Joseph Butore, huku serikali ya Sudan Kusini ikiwakilishwa pia na makamu wa pili wa rais, James Waniiga.

Na katika hatua nyingine kikao hicho kimepitisha jina la Liberate Mfumukeko kutoka Burundi kuwa katibu mkuu mpya wa jumuiya  hiyo kuanzia Aprili 1 mwaka huu.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree