Wednesday, 2 March 2016
Jifunzeni kusamehe na kusahau!
Posted by Unknown on 23:39:00 in | Comments : 0
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 1 Machi 2016 amesema kwamba, Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; muda muafaka wa kuonja huruma na upendo wa Mungu; tayari kusamehe na kusahau kama Kristo anavyofundisha katika Injili na Sala ya Baba Yetu. Hii ni changamoto ambayo inafumbatwa katika Liturujia ya Neno la Mungu.
Yesu anapoulizwa na Mtume Petro anaweza kumsamehe mara ngapi ndugu yake aliyemkosea; Sala ya Azaria aliyechomwa moto kwa kukataa kuabudu ndama wa dhahabu, akiwa katikati ya tanuru la moto anaomba huruma ya Mungu kwa ajili ya watu wa Mungu sanjari na kuomba msamaha wa dhambi zake. Huu ndio mwelekeo sahihi wa kusali anasema Baba Mtakatifu Francisko, ili kuambata huruma, upendo na wema wa Mungu katika maisha.
Msamaha wa Mungu hauna mipaka na kamwe hauweki kisasi, changamoto na mwaliko kwa waamini kutoweka kisasi katika mioyo yao, wawe tayari kuomba huruma ya Mungu ili aweze kuwaokoa. Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kuhurumia na kumwokoa mdhambi.
Yesu katika Injili anawaalika wafuasi wake kujenga utamaduni wa kusamehe na kusahau na kamwe wasiwe wepesi kulipiza kisasi kama inavyojionesha kwa mdaiwa asiye na huruma, baada ya kuhurumiwa, lakini yeye anashindwa kumrehemu mjoli wake. Sala ya Baba Yetu inamwelekeo kama huu, waamini wanamwomba Mungu aweze kuwahurumia dhambi zao, lakini kwa baadhi ya waamini wanajikuta wakiwa na moyo uliofungwa katika ubinafsi, kiasi hata huruma haiwezi kupenyeza, kiasi hata cha kusema, nimekusamehe, lakini sitasahau hata kidogo!
Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kuomba neema ya Mungu ili aweze kuwasaidia kurehemu na kusahau kama afanyavyo Mwenyezi Mungu. Hii ni huruma na upendo wa Mungu unaosamehe na kusahau. Waamini wanarehemiwa na Mungu wawe tayari pia kuwasamehe ndugu zao. Waamini wawe wepesi kuomba huruma ya Mungu katika maisha yao na kuwagawia pia jirani zao kwani Mwenyezi Mungu anaposamehe anasahau pia.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment