BREAKING NEWS

Saturday, 12 March 2016

Rais Magufuli Atuma Salamu Za Rambirambi Kwa Rais Shein Kifo Cha Mzee Ibrahim Amani


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha mmoja wa wanamapinduzi, Mzee Ibrahim Amani Kilichotokea jana tarehe 11 Machi, 2016 Mjini Unguja.
 
Mzee Ibrahim Amani ambaye aliwahi kuwa Waziri na Mjumbe wa baraza la Mapinduzi Zanzibar, ni mmoja wa Watu 14 waliojitoa muhanga kupambana na kuuondoa utawala wa kisultani huko Tanzania Zanzibar, na kuondoka kwake kunafanya idadi ya wanapinduzi waliotangulia mbele za haki kufikia 13.
 
Katika Salamu zake, Rais Magufuli amesema kwa mara nyingine Taifa limepoteza mtu muhimu, Mzalendo wa kweli na ambaye daima alisimama kidete kutetea Taifa lake dhidi ya vitendo vyenye kuleta madhara.
 
“Nimeguswa sana na kifo cha Mzee Ibrahim Amani, maisha yake na nia yake ya kupigania uhuru na uzalendo kwa taifa lake ni mambo ambayo daima tutayaenzi” Amesema Rais Magufuli.
 
Dkt. Magufuli amemuomba Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kumfikishia salamu za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na kifo cha Mzee Ibrahim Amani.
 
“Tumwombe Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Ibrahim Amani mahali pema peponi, Amina.” Amemalizia Rais Magufuli.
 
Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
12 Machi, 2016.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree