
WAKUU
wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameazimia Rais John
Magufuli awe Mwenyekiti wa jumuiya, kwa maana kwamba Tanzania iendelee
mwaka mwingine kuongoza kipindi ambacho Burundi ndiyo ilipaswa kushika
wadhifa.
Dk
Magufuli ambaye anaongoza jumuiya hiyo ambayo imepata mwanachama
mwingine, Sudan Kusini, ameanza kwa kasi kubwa huku akipenyeza msimamo
na falsafa yake ya ‘kutumbua majipu’ kuhakikisha nchi wanachama
wanakwenda pamoja na kuleta maendeleo ya wananchi.
Hayo
yalifanyika katika mkutano wa kawaida wa 17 wa Jumuiya, ambapo wakuu
hao wa nchi pia walikubaliana kwa pamoja Rais mstaafu, Benjamin Mkapa
kushirikiana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kutatua mgogoro wa
Burundi.
Magufuli
aliahidi atafuatilia Sekretarieti ya EAC, kuhakikisha inafanya kazi kwa
maslahi ya wananchi wa nchi wanachama na si kuwanyonya.
Rais
Magufuli alihimiza viongozi wakuu wa umoja huo, kutoa kipaumbele katika
ujenzi wa viwanda. Alisisitiza msimamo wake kupitia Sekretarieti ya
jumuiya hiyo, kubana matumizi kuhakikisha malengo ya kuleta maendeleo
katika nchi wanachama yanatimia.
Akizungumzia
gharama za ukumbi waliotumia kwa ajili ya mkutano huo wa 17 kwenye
Hoteli ya Ngurdoto, Magufuli alisema dola 45 kwa kichwa zilizotumika ni
nyingi ambazo kama zingebanwa, zingeokoa fedha ambazo zingenunua
madawati na kwenda kusaidia mahali pengine.
“Mwito wangu kwa sekretarieti, muwe cost conscious (macho na gharama),” alisema.
“Tubane sana matumizi iwezekanavyo, tukahudumie watu masikini na si kuwa na Sekretarieti inayokuwa parasite (nyonyaji),” aliendelea kusema.
Sekretarieti
hiyo inaongozwa na Liberal Mfumukeko kutoka Burundi, aliyeteuliwa na
wakuu hao wa nchi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka
mitano baada ya Dk Richard Ssezibera wa Rwanda, muda wake kumalizika.
Magufuli
katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, alisema amepiga hesabu
ukumbi huo ni ghali. Alitoa mwito kwa sekretarieti na watumishi wote
kwamba ni lazima wafahamu kwamba wako kwa watu masikini na wanahudumia
watu masikini katika nchi wanachama.
“Nataka
niiambie Sekretarieti, Marais wamefanya kosa sana kunichagua mimi kuwa
mwenyekiti. Nitahakikisha nawafuatilia kweli. Kwa hiyo mjipange vizuri
na kama patakuwapo mmoja wa wafanyakazi anakwenda sehemu isiyotakiwa,
nitaripoti kwa nchi anakotoka ili atumbuliwe jipu,” alisema.
Alisisitiza
ifanye kazi kwa niaba ya nchi zao kwa kutengeneza sheria na mambo
yatakayozisaidia. Alihimiza sekretarieti isiwe sehemu ya walalamikaji,
bali wawe watatuzi wa matatizo ya jumuiya.
Alisema
nchi wanachama wanapaswa kubadilika, kuwa na mtazamo wa kuhakikisha
wananchi wake wananufaika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tunapaswa kutembea pamoja kwa maslahi ya jumuiya,”
alisema. Rais Magufuli anaongoza jumuiya hiyo kwa mwaka mmoja, nafasi
ambayo ilipaswa sasa ichukuliwe na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.
Hali
hiyo inatokana na nchi hiyo kuomba kuachia nafasi hiyo ili kuelekeza
nguvu zake katika kushughulikia matatizo yake ya ndani, lakini ilipewa
nafasi ya kutoa Katibu.
Jumuiya
ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda
na Burundi huku Sudan Kusini ikiwa imekidhi vigezo na kukubaliwa kuwa
mwanachama mpya wa jumuiya hiyo katika mkutano huo wa 17.
Post a Comment