
TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza, imemfikisha
mahakamani aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata (63) na
wenzake wawili wakikabiliwa na mashitaka ya kutumia vibaya madaraka.
Washitakiwa
wengine katika kesi hiyo waliofikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi wa Wilaya ya Nyamagana ni aliyekuwa Mhandisi wa Manispaa ya
Ilemela, Justine Lukaza (42) na mfanyabiashara Hemedi Hamad (54).
Mwendesha
Mashitaka wa Takukuru, Mwema Mella, alidai mbele ya hakimu Greyson
Sumaye kwamba kati ya Juni mosi na Julai 31, mwaka 2014, washitakiwa hao
walitumia vibaya madaraka kwa kutoa zabuni ya kutoza ushuru katika
Kituo cha Mabasi cha Buzuruga kinyume cha utaratibu.
Alifafanua
kuwa makosa waliofanya ni kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa mamba 11/2007 na pia walikiuka sheria ya
manunuzi ya umma namba 7/2011
Wakati
kesi hiyo inafikishwa mahakamani jana, mshitakiwa Lukaza hakuwepo,
hatua iliyomfanya Mwendesha Mashitaka kuomba mahakama hati ya kumkamata.
Hakimu
aliridhia ombi hilo na kesi hiyo ilioahirishwa hadi Machi 29 mwaka huu.
Washitakiwa wawili waliokuwepo mahakamani walikana mashitaka hayo na
wako nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Post a Comment