Saturday, 12 March 2016
Msamaha ni chombo kilichowekwa katika mikono dhaifu
Posted by Unknown on 20:20:00 in | Comments : 0
Ndugu zangu wapendwa, tunamshukuru tena Mungu Baba Mwenyezi kwa kutupatia tena fursa ya kutafakari neno lake. Tunaadhimisha dominika ya 5 ya kwaresima. Dominika iliyotangulia tulisikia habari juu ya kukubali na kukiri kosa. Katika mengi tuliyosikia tukakumbushwa kuwa msamaha ni tendo linalotoka ndani na juhudi za kukubali, kukiri na kutaka msamaha zinatoka kwa mtenda tendo. Lakini tukaona kuwa ili msamaha ukamilike ni lazima aliyetendewa ampokee mkosaji.
Habari ya Baba mwenye huruma na mwana mpotevu ikatupatia changamoto kubwa. Katika Mt. 18:21 – kuhusu kusameheana tunasoma hivi, kisha Petro akamwendea, akasema, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Mtume Petro hakusema aliyenikosea aniombe msamaha mara ngapi. Tukaona kuwa tendo halisi la upatanisho hutoka kwa Mungu, kwa njia ya mwanawe na mtume Paulo anasema kuwa naye Mungu anatupa sisi huduma ya upatanisho – 2Kor. 5:18. Na tukaalikwa tukasemeheane makosa yetu.
Leo tunaona wazi kuwa kuna mwendelezo wa ujumbe wa neno hilo la Mungu. Yule aliyesamehe na aliyesamehewa wanaalikwa kuanza maisha mapya. Hii ndiyo dhamira ya neno la Mungu dominika hii ya 5, kuanza upya.
Tunasikia katika somo la pili Mtume Paulo anatamani kumjua yeye na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake. Anatamani kufananishwa na kufa kwake. Haya maneno au ni ya kichaa au ya mtu mtakatifu. Mtu mwingine angeweza kusema/kuomba kufunguliwa au kuachana na njia ya Kristo. Sitaki kuteseka na kufa. Paulo anasema yote ni mavi, yote ni ubatili. Paulo atualika tufahamu, lakini siyo ufahamu wa kujua suluhu ya tatizo fulani kama vile kupata jibu la tatizo fulani bali aongelea uzoefu wa ndani.
Mambo matatu makuu katika ufahamu huu; katika kumjua Kristo, kuijua nguvu ya ufufuko wake, kushiriki ufufuko wake na kumjua Kristo mfufuka anayeshirikisha uweza wake kwao wamwaminio na wanaopenda kuwa naye. Paulo anafikia hatua ya kuita mambo mengine yote ni ubatili, mavi. Aidha Mtume Paulo anatualika tupige mbio – ninapiga mbio, niifikie tuzo ya juu aliyoniweea Mungu katika Kristo Yesu.
Katika somo la kwanza twaona Mungu ataumba upya na nabii Isaya anaweka wazi matumaini hayo mapya mbele ya watu wake. Kanisa laelewa huko kuumbwa upya kutafanyika katika Kristo. Ndicho anachoongelea Mtume Paulo katika somo la pili na ndiyo wito wetu leo.
Injili yaongelea juu ya upya. Amri ya zamani – mzinzi anauawa. Amri mpya, mzinzi anasamehewa. Huku ndiko kuumbwa upya. Ni zaidi ya maagizo ya sheria. Huruma inachukua nafasi juu ya sheria. Isionekana kuwa Yesu anaunga mkono kosa la yule mama. Neno la mwisho kwa yule mama, usitende dhambi tena laonesha wazi kuwa Yesu haungi mkono tendo hilo. Kinachonekana wazi hapa ni kuwa uwepo wa Yesu hubadilisha umauti wetu. Akiwepo Mungu, huwepo uzima. Na hii ndiyo hali yake Mungu. Anatuweka huru – Yoh. 8:11. Hapa Yesu anasimama kinyume che sheria. Hapa anapata upinzani mkubwa. Leo tunapata nafasi ya kuona jinsi Yesu anavyotuonesha huruma yake ambayo inatuwajibisha sisi ambao tayari tulishahukumiwa kwa sababu ya dhambi zetu.
Wakati fulani Jean Jacques Rousseau alipokuwa anawindwa kila kona sababu ya mawazo yake mabaya, Voltaire alisikia na ingawa hakuunga mkono hayo mawazo yake alimpokea nyumbani kwake na kumpa hifadhi. Alisema ingawa sikuingi mkono katika mawazo yako lakini nitakulinda katika haki yako au katika uhuru wako wa kusema. Bila shaka kwa kumpa hifadhi, alimpatia nafasi ya kuangalia au kutafakari kile alichokuwa anasema.
Ndugu zangu, ili neno hili lieleweke na kutuwajibisha katika tafakari za maisha yetu, hatuna budi kujiweka upande wa yule mwanamke mzinzi. Kama Yule mwanamke, sote tumetenda dhambi – Rum. 3:23 na kama yeye sote tunapaswa adhabu ya kifo – Rum. 6:23. Katika ufahamu huu sisi tunaalikwa kuutambua ukuu na huruma ya Mungu. Leo tunawajibishwa na historia nzima ya wokovu kama ilivyoletwa kwetu na Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu.
Mtakatifu Augustino anasema Mungu ametuumba sisi bila hiari yetu, lakini kuupata wokovu yahitaji juhudi binafsi. Tuombe tena leo ili neema ya Mungu iendelee kutawala na sote tuweze kuendelea kusema ufalme wako ufike. Tuendelee kuomba mwanga wa roho mtakatifu ili tuweze kuuona utukufu wa Mungu kati yetu. Tunaamini kuwa neema hii ikiwepo kati yetu basi wajibu wetu wa kwanza utakuwa ni kuzuia na kuepuka nafasi za dhambi ili tusitenda dhambi tena.
Tumsifu Yesu Kristo.
Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment