Wednesday, 16 March 2016
Msalaba Mtakatifu ni kielelezo na ushuhuda wa upendo wa Mungu!
Posted by Unknown on 22:09:00 in | Comments : 0
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 15 Machi 2016 anasema, ikiwa kama waamini wanataka kuona na kushuhudia historia ya upendo wa Mungu kwa mwanadamu hawana budi kuangalia Msalaba Mtakatifu, pale Mwana wa Mungu alipochafuliwa kwa dhambi, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Neno la Mungu linamwonesha nyoka kuwa ni kiumbe wa ajabu na mwenye nguvu na akili nyingi kiasi hata cha kumvuruga mwanadamu.Maandiko Matakatifu yanasimulia jinsi ambavyo Waisraeli walichoka na safari wakakikinai chakula walichopewa na Mungu wakiwa njiani kuelekea kwenye nchi ya ahadi. Matokeo yake Waisraeli wakamlalamikia Musa na Mwenyezi Mungu na hapo Mungu akakasirika na kuwaonesha cha mtema kuni kwa kuumwa na nyoka! Watu waliokosa uaminifu, wakashikwa na butwaa na kumkimbilia tena Musa, ili kumwomba aweze kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili kuwaondolea balaa la nyoka na madhara yake.
Ili kuwaokoa Waisraeli waliokuwa wameng’atwa na nyoka, Musa alitengeneza nyoka wa shaba na kumtundika juu na kila mtu aliyekuwa ameng’atwa na nyoka alipomtaza yule nyoka wa shaba akapona. Baba Mtakatifu anashangaa na kusema, Mwenyezi Mungu anamwacha nyoka aendelee “kutanua tu katika historia”. Neno “kumsimamisha” lina maana ya pekee katika maisha na utume wa Yesu anayewaambia Mafarisayo na waandishi kwamba, Mwana wa mtu akishainuliwa, watamtambua kwamba Yeye ndiye, jina ambalo linaonesha pia ufunuo wa Mungu kwa Waisraeli.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, nyoka ni alama ya dhambi; nyoka ni alama ya kifo, lakini pia nyoka ni alama inayoleta uzima mpya, hiki ndicho kiini cha Fumbo la Kristo Yesu ambalo Mtakatifu Paulo analifafanua kwamba, Yesu kwa njia ya mateso na kifo chake, aliyamimina maisha yake, akajinyenyekesha na kujitwalia hali ya ubinadamu, katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi!
Yesu akachafuliwa na dhambi, lakini aliponuliwa pale juu Msalabani akawa ni chemchemi ya maisha mapya. Hii ndiyo historia ya ukombozi, historia ya upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Upendo wa Mungu umefumbatwa katika Fumbo la Msalaba, pale ambapo Kristo aliyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kwa njia ya Damu yake azizi akavunjilia mbali nguvu za shetani!
Yesu kwa kuinuliwa pale Msalabani amewainua waja wake wote. Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha sadaka ya Mungu kwa ajili ya upendo kwa binadamu. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, Mungu anamponya na kumkomboa mwanadamu!
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment