BREAKING NEWS

Wednesday, 9 March 2016

Jipe moyo! Inuka, anakuita!



 Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 4 Machi 2016 ameadhimisha Mpango mkakati wa saa 24 kwa ajili ya Bwana kwa kuungama na kuungamisha katika Ibada ya Upatanisho iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Zaidi ya Mapadre 70 wameshiriki kuungamisha waamini waliokuwa wamehudhuria katika Ibada hii ambayo kwa sasa inaingia mwaka wake wa tatu! Katika tukio kama hili, mwaka 2015, Baba Mtakatifu Francisko alitangaza nia yake ya kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaka ambao kwa sasa unaendelea kupamba moto kwa himizo la toba, wongofu wa ndani na matendo ya huruma kiroho na kimwili!

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu alifanya rejea kwenye Injili ya Marko pale mwana wa Timayo, Bartimayo kipofu alipomwambia Yesu, mwalimu wangu, nataka nipate kuona! Kwa kutenda dhambi mwamini anashindwa kuona na kuitikia vyema wito wake, kiasi cha kushindwa kufikia lengo la maisha. Upofu wa Bartimayo, ulimfanya kutelekezwa na Jamii kama ilivyo dhambi inayomfukarisha mwamini na kumsababishia upofu wa moyo, kiasi hata cha kushindwa kuona mambo msingi katika maisha kwa kuwa na mwelekeo potofu kuhusu upendo na maisha na hatimaye kutowajali wengine.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, vishawishi vinaufanya moyo wa mwanadamu kuwa na upeo mfinyu wa kuona mambo na kudhani kwamba maisha ya mtu yanayotokana na vitu alivyo navyo; mafanikio ya maisha au pongezi na sifa anazojinyakulia mbele yajamii. Watu wanadhani kwamba, uchumi unajikita kwa kupata faida kubwa hata wakati mwingine mafao binafsi yanapewa kipaumbele cha kwanza badala ya ustawi na maendeleo ya wengi. Haya ni matokeo ya mtu kujitafuta na kuzama katika ubinafsi, hali inayomfanya kuwa kipofu wa moyo na mtu asiye kuwa na furaha na uhuru katika maisha! Jambo ambalo linatia kichefu chefu kabisa!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu aliposikia sauti ya Bartimayo kipofu, alisimama,  akamwangazia mwanga wa huruma, unaomwokoa mwanadamu kutoka katika giza na upofu wa moyo kwa kuonesha uwepo wake wa karibu, ambao ni muhimu sana katika maisha ya mwamini. Hapa mwamini anajisikia kuwa kweli anahitaji wokovu, mwanzo wa mchakato wa uponyaji wa roho na hatua kwa hatua, mtu anapaaza sauti yake kwa njia ya sala, ili kuomba msaada kama alivyofanya Bartimayo kipofu kwa kupiga kelele, Yesu mwana wa Daudi unihurumie!
Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, kama ilivyokuwa wakati ule wa Yesu, kuna watu ambao hawataki kusikia sauti ya watu wanaolalama kutokana na mateso na masumbuko yao ya ndani; hawa wangependa kuona watu hawa “wanafyata mkia” na kukaa kimya. Watu wanataka kuendelea mbele kana kwamba, hakuna jambo lolote lililotokea, ili waweze kuwa mbali na Yesu pamoja na jirani kadiri inavyowezekana.
Lakini waamini wakumbuke kwamba, wao wote ni waombaji wa upendo wa Mungu na kwamba, kamwe hawatapotea kutoka katika macho yake pale anapopita. Kwa kawaida wanaogopa kusikia kwamba Yesu anapita! Changamoto hapa ni kupiga ukelele kama alivyofanya Bartimayo kipofu, mwalimu wangu nataka kuona tena! Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi muafaka cha kupokea na kuambata upendo na uwepo endelevu wa Mungu katika maisha, tayari kumrudia tena kwa moyo wote kama alivyofanya Bartimayo kipofu, aliporuka na kutupa kando vazi lake, akamkimbilia Yesu.
Huu ni mwaliko kwa waamini kutupilia mbali mambo yote yanayowakwamisha kumwendea Yesu, wawe na ujasiri wa kusimama imara ili kutambua utu wao kama watoto wapendwa wa Mungu, ili kuangaliwa, kusamehewa na kupewa tena maisha mapya! Simama ndio mwaliko ambao unatolewa na Mungu kwa waja wake wakati huu! Viongozi wa Kanisa wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kusikiliza kilio cha watu wanaotaka kuonana na Kristo Yesu.
Ratiba na mipango ya shughuli za kichungaji isaidie waamini kukutana na Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili wasamehewe dhambi zao. Ugumu wa mioyo ya wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho unaweza kuwa ni kikwazo kikuu cha waamini kukutana na huruma ya Mungu. Kuwepo na mipango thabiti ili kukidhi mahitaji ya Uinjilishaji na kutoa nafasi kwa waamini kujipatanisha na Mungu anayemsubiri mdhambi ili aweze kutubu na kumwongokea tena!
Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kurudia tena maneno  ambayo Mitume wa Yesu walimwambia Bartimayo kipofu, “Jipe moyo, Inuka, anakuita!”. Wahudumu wa Injili watambue kwamba, wanatumwa duniani kuwatia watu shime na kuwaongoza ili kumwendea Yesu, ili kweli kila mtu aweze kukutana ana kwa ana na Yesu mwenyewe, ili kuwasikiliza, kuwaganga na kuwaponya waja wake. Viongozi wa Kanisa wasaidie kuwahamasisha watu kutubu na kumwongokea Mungu, ili watu waonje kweli huruma na upendo wa Mungu.
Sakramenti ya Upatanisho iwe ni mahali ambapo mwamini anakutana na Baba mwenye huruma anayemsubiri, anayesamehe na kusahau. Baada ya kuponywa na kugangwa na Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, waamini wawe na ujasiri wa kumfuasa Yesu ili kuambatana naye kwani mtu anaye amini, huyo ana uwezo wa kuona na kusonga mbele kwa imani na matumaini kwani anatambua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye, anamuenzi na kumwongoa. Huu ni mwaliko wa kumfuasa kama wafuasi amini, ili kuweza kuwashirikisha wengine hija ya maisha ya furaha na huruma ya Mungu. Baada ya kuondolewa dhambi, basi mioyo ya waamini ifurahi kwani Mungu ndiye anayewakirimia furaha hii katika mioyo yao!

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree