BREAKING NEWS

Tuesday, 22 March 2016

CUF Yatangaza Kutoyatambua Matokeo ya Uchaguzi wa Marudio Zanzibar....Pia Haitambui Ushindi wa Dr Shein


Kufuatia ubakaji wa demokrasia kupitia kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio uliofanywa juzi tarehe 20 Machi, 2016, jana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alikamilisha kazi aliyoagizwa kwa kutangaza kile alichokiita matokeo ya uchaguzi wa Urais.

Chama Cha Wananchi (CUF) kilishaeleza msimamo wake kuhusu ubakaji huo wa demokrasia kupitia taarifa yake kiliotoa tarehe 18 Machi, 2016. Baada ya hatua ya jana tunaweka msimamo wetu kwamba:

1. Hatutambui hicho kinachoitwa matokeo ya uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016 na kwa maana hiyo hatumtambui huyo aliyedaiwa kuwa mshindi na kwa msingi huo huo hatutoitambua wala kushirikiana na Serikali itakayoundwa kutokana na matokeo hayo batili ya uchaguzi batili.

2. Tunawapongeza kwa dhati Wazanzibari wote kwa ukomavu wao mkubwa wa kisiasa waliouonesha kwa kuitikia wito wa mpendwa wao Maalim Seif Sharif Hamad na chama chao cha CUF na kutoshiriki katika uchaguzi huo batili. Kwa ujasiri wao huo wameudhihirishia ulimwengu kwa njia za amani na za kistaarabu kwamba chaguo lao ni Maalim Seif Sharif Hamad. Kwa mara nyengine tena Wazanzibari wameyathibitisha maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya kupitia uchaguzi huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

3. Tunavipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje na jumuiya ya kimataifa kwa kuonesha hali halisi ilivyokuwa na jinsi Wazanzibari walivyoikataa CCM, walivyowakataa watawala na walivyokataa kutumika kubaka demokrasia. Wazanzibari wameandika historia nyengine mbele ya macho ya ulimwengu. Kwa mara nyengine tena Wazanzibari wameshinda.

4. Tunajua Wazanzibari wana hamu ya kujua hatua zinazofuata katika kusimamia maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015. Chama chao kinawatoa wasiwasi Wazanzibari kwamba hakijayumba na kinafuatilia haki yao hiyo kwa njia za amani na za kidemokrasia na kitakuwa kikiwaeleza kila kinachoendelea.

HAKI SAWA KWA WOTE

NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU – CUF
22 Machi 2016

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree