Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema imeanza
kutekeleza mikakati mipya ya ukusanyaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka
kwa wadaiwa ambayo itaongeza wastani wa ukusanyaji wa Tshs 2.6 bilioni
za sasa hadi kufikia Tshs 8 bilioni ifikapo mwezi Julai mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry Sabi ameyasema hayo jana (Jumatano, Machi 30, 2016) jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyotembelea ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mwenge.
“Hadi
mwezi uliopita (Februari, 2016) tulikuwa tunakusanya wastani wa
shilingi bilioni 2.6 kwa mwezi, lakini sasa tumeongeza kasi na mikakati
mipya ambayo itawezesha kukusanya shilingi bilioni 6 mwezi Aprili na
shilingi bilioni 8 ifikapo mwezi Juni mwaka huu,” alisema Bw. Sabi aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo na miezi miwili iliyopita.
HESLB ilianzishwa ilianza kazi mwaka 2005 ili kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na pia kukusanya mikopo kwa wanufaika.
Hadi
sasa, zaidi ya shilingi 2.1 trilioni zimetolewa kwa wanufaika na kati
ya fedha hizi, mikopo iliyoiva na inayopaswa kukusanywa ni shilingi 258
bilioni ambazo wanufaika wake wamemaliza au kusitisha masomo yao na
vilevile kumaliza muda wa kujipanga kuanza kulipa (grace period).
Kwa
mujibu wa Bw. Sabi, hadi sasa, HESLB imekusanya shilingi 91 bilioni
kati ya shilingi 258 bilioni zilizoiva na hivyo kupaswa kukusanya.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji huyo alikuwa akijibu hoja zilizotolewa na Wajumbe
wa Kamati hiyo waliokutana na watendaji wa Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na HESLB wakiongozwa na Waziri Prof.
Joyce Ndalichako na Naibu wake Mhandisi Stella Manyanya.
Bw.
Sabi alitaja mikakati mipya iliyobuniwa na HESLB kuwa ni pamoja na
kuimarisha mtandao baina ya Bodi na waajiri kutoka sekta binafsi na umma
ambao unalenga kubaini na kukusanya kiasi cha shilingi 7.02 bilioni kwa
mwaka kutoka kwa wanufaika 136,252.
“Tunapata
ushirikiano mkubwa kutoka kwa taasisi za Serikali na sasa tumejipanga
kupitia upya mitandao ya waajiri kwa kushirikiana na taasisi kama Chama
cha Waajiri (ATE), Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF) na Shirikisho la Asasi
zisizo za Kiserikali (TANGO) ili kuhuisha takwimu zetu kuhusu waajiri
ili kukusanya taarifa za wadaiwa wapya kwa haraka,” alifafanua Bw. Sabi.
Mikakati
mingine ni kutoa elimu na kuimarisha ushirikiano na wadau mahsusi kama
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Mashirika ya
Hifadhi za Jamii (SSRA), Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), Kituo
cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa
Hesabu Tanzania (NBAA) na vyama vya kitaaluma.
Akizungumza
katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mbunge wa
Kigoma Kaskazini Bw. Peter Serukamba ameitaka HESLB kuongeza kasi ya
kudai mikopo iliyoiva na kuutaka uongozi wa HESLB kuandaa orodha ya
wadaiwa wote na kuiwasilisha kwa kamati ili ifanyiwe kazi.
“Ni
lazima kuwe na fedha ili kuwezesha kutoa mikopo kwa wahitaji wengine
...haiwezekani mtu anapata mkopo halafu halipi...andaeni orodha ya wote
walionufaika na mikopo ambayo itaonyesha nani halipi, nani analipa na
nani amemaliza na tutaamua tufanye nini,” alisema Sekukamba.
HESLB
ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai mwaka 2005 kwa
lengo la kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji waliopata nafasi za masomo
katika vyuo vya elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa
wadaiwa walionufaika na mikopo tangu mwaka 1994.
Baadhi
ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii
wakibadilishana mawazo na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi Prof. Joyce Ndalichako (katikati) wakati Kamati hiyo
ilipotembelea ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) jijini Dar es Salaam
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Bi.
Maimuna Tarishi akisalimiana na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Maendeleo ya Jamii Dkt. Ely Macha (kulia) wakati Kamati hiyo
ilipotembelea ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) jijini Dar es Salaam jana (Jumatano, Machi 30, 2016). Katikati
mwenye suti ya kijivu ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry
Sabi.
Post a Comment