MKUU
wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela ametoa siku sita kwa
Wakurugenzi wa Halmashauri tatu za Ushetu, Msalala na Kahama zilizopo
wilayani Kahama kuhakikisha wanawakilisha kwake majina ya watumishi hewa
ifikapo Jumatano ijayo.
Mkuu
huyo wa Mkoa aliyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa
halmashuri zote tatu za Wilaya ya Kahama muda mfupi baada ya kumaliza
ziara yake ya siku moja ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani
Kahama, ikiwa ni sambamba na kuwapa pole waathirika wa mvua kubwa ya
mawe katika kijiji na Kata ya Mwakata.
Mvua
hiyo ya mwanzoni mwa Machi mwaka jana ilisababisha maafa makubwa, ikiwa
ni pamoja na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 38 na kujeruhi wengine
zaidi ya 80.
Kilango
alisema lundo la watumishi hewa katika halmashauri hizo halikubaliki,
hivyo ni wajibu wa wakurugenzi kuhakikisha kuwa majina yao
yanawakilishwa ofisi ya mkuu wa mkoa sambamba na maelezo ya kumbukumbu
zao za ajira, wanavyolipwa na kiasi wanacholipwa.
“Hata wakurugenzi wakiwaficha, tayari orodha yao ninayo mezani…naomba mniletee majina,” alisema mkuu huyo wa mkoa aliyeanza kazi hivi karibuni baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli.
Katika Awamu iliyopita ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Anne Kilango alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Pia
aliwataka viongozi wa halmashauri hizo kuhakikisha wanaongeza kasi ya
kukusanya mapato, ikiwa ni sambamba na kuongeza weledi ili mapato hayo
yasipotee.
“Maendeleo
ya Kahama yanatuhusu wote. Sipendi kumsimamisha mtu kazi kwa tuhuma za
ubadhirifu, lakini ikibidi kufanya hivyo nitafanya kulingana na kasi ya
uongozi wa Serikali ya Awamu Tano chini ya uongozi wa Rais John
Magufuli,” alisema.
Post a Comment