WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema ataitisha kikao cha viongozi wa dini zote hivi
karibuni ili wapange na kuainisha ni mambo gani ambayo wanaweza kutoa ushauri
kwa Serikali na kupata njia bora ya kuwahudumia Watanzania.
Ametoa
ahadi hiyo leo mchana (Jumapili, Februari 7, 2016) wakati akizungumza na mamia
ya waumini walioshiriki ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Pili wa Kanisa la
Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Askofu Dk. Brown Abel
Mwakipesile iliyofanyika kwenye kanisa la EAGT la Mlimwa West nje kidogo ya mji
wa Dodoma.
Waziri
Mkuu Majaliwa ambaye alihudhuria ibada hiyo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe
Magufuli alisema: “Hivi karibuni nitaitisha kikao cha viongozi wa dini zote
kitakachojumuisha Maaskofu Wakuu, Masheikh na baadhi ya wachungaji ili tukae na
kubaini ni nini kifanyike ili kuisadia Serikali namna nzuri ya kuboresha maisha
ya Watanzania.”
Akijibu
risala iliyosomwa na Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Leonard Mwizarubi, Waziri
Mkuu alisema Serikali imeanza kufanya mapitio ambayo yatawawezesha Watanzania
kupata huduma kwa urahisi.
“Katibu
Mkuu pamoja na Baba Askofu Mkuu wamegusia suala la upandaji wa gharama za vifaa
vya ujenzi pamoja na suala la makazi bora. Mwezi ujao tunaanza vikao vya Bunge
vya kupitia bajeti ya Serikali, tutaliangalia hili kwa kumshirikisha Waziri wa
Fedha… tutafanya mapitio katika hili ili mwananchi wa kawaida aweze kumudu
maisha,” alisema huku akishangiliwa na waumini hao.
Aliwaomba
viongozi wa kanisa hilo pamoja na waumini wake waendelee kuiombea nchi pamoja
na viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwani kazi ya kutumbua majipu
waliyoianzisha ina mitihani mikubwa.
“Kutokana
na maombi yenu kwa viongozi wakuu wa kitaifa nina imani Taifa hili litafika
tunakotaka liende. Endeleeni kutuombea kwa sababu kazi ya kutumbua majipu ina
mitihani mikubwa. Lakini pia napenda niwahakikishie kuwa Serikali hii itatumbua
majipu hayo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Hakuna mtu
ambaye ataonewa,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Kuhusu
mgogoro wa kiwanja cha kanisa hilo kilichopo eneo la Ipagala, Waziri Mkuu
aliahidi kulishughulikia suala lao kesho asubuhi kabla hajaondoka kurejea Dar
es Salaam. “Kesho asubuhi nitamuita Mkurugenzi Mkuu wa CDA na kumtaka anipe
taarifa sahihi kuhusu mgogoro huu. Najua suala hili liko mahakamani, lakini
naamini Mkurugenzi anaweza kuwa kiungo kizuri kati ya wananchi waliojenga eneo
hili pamoja na kanisa ambao mnamiliki kiwanja husika”.
“Kama
atapata eneo jingine na kupima viwanja, kisha akawapatia hawa wananchi anaweza
kuwa amesaidia kuondoa mgogoro huu. Wananchi walienda mahakamani huku wakijua
eneo lenu limewekewa uzio, sasa wanagoma kutoka kwa sababu hawana mahali pa
kwenda,” aliongeza.
Mapema, akitoa hotuba yake, Askofu Mkuu Dk.
Mwakipesile alisema kanisa litaendelea kuiombea Serikali ya awamu ya tano ili
nchi idumu katika amani na utulivu.
Aligusia
eneo la kanisa lililopo kiwanja na 34, kitalu ‘E’, Ipagala East, Dodoma, ambalo
ujenzi wa shule yake umesimama kutokana na mgogoro baina yao na wananchi waliovamia
eneo lao kwa kujenga nyumba za kuishi licha ya kuwa eneo hilo lilikwishawekewa
uzio.
“Kama
kanisa tumeshindwa kukamilisha ujenzi wa shule kwa sababu wananchi hao
walifungua kesi mahakamani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Tunaomba uamuzi wa
kesi hii uharakishwe,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema
kanisa hilo lina majengo 4,670 nchini kote na viwanja 420 ambavyo ni vya
kujenga makanisa na vituo vya kutoa huduma mbalimbali za kijamii.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk.
Mwizarubi alisema katika risala yake kwamba wanaiomba Serikali ifikirie
kushusha bei ya vifaa vya ujenzi ili wananchi waweze kuwa na nyumba bora za
kuishi.
“Maisha
bora maana yake ni kuwa na nyumba bora. Tunaiomba Serikali yako ipunguze bei ya
vifaa vya ujenzi ili Watanzania waweze kuwa na makazi bora,” alisema huku
akishangiliwa.
Post a Comment