Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
leo amekuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupinga
Ukeketaji Duniani yanayofanyika tarehe 5 Februari kila mwaka.
Maadhimisho hayo kwa Mkoa wa Dodoma yalifanyika katika Ukumbi wa Hazina
Dodoma, kwa kuratibiwa na Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
yanayopinga Ukeketaji Tanzania.
Wakati wa
maadhimisho hayo Mhe Waziri Ummy Mwalimu alieleza kuwa Kwa mujibu wa
Takwimu za Demografia na Afya Tanzania (Tanzania Demographic and Health
Survey – TDHS 2010) asilimia 15 ya wanawake Tanzania wamefanyiwa
Ukeketaji. Ukeketaji ni ukatili dhidi ya watoto wa kike na wanawake. Na
ni kosa la jinai. Madhara ya ukeketaji ni pamoja na vifo, vilema na
maradhi kama fistula na mengineyo.
Alieleza
kuwa Serikali itaendelea kukemea na kupambana na vitendo hivi katika
jamii zetu. Na itaongeza jitihada za kutoa elimu kwa jamii sambamba na
kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na vitendo hivi.
Mhe Waziri Ummy Mwalimu aliwataka Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Mikoa.
Wilaya na
Kata kuongeza nguvu ktk kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa lengo la
kuhakikisha wazazi/walezi, mangariba na wote wanaojihusisha na vitendo
vya Ukeketaji wanafikishwa ktk vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo
wake.
Aidha, alitoa wito kwa kila mwananchi kushiriki katika mapambano haya hasa katika kutoa taarifa na ushahidi Mahakamani.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akipokea maandamano ya wadau
mbalimbali wa Maendeleo ya Mtoto katika viwanja vya ofisi za Hazina
Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya kupinga ukeketaji kwa wanawake
na watoto wa kike.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akihutubia wadau mbalimbali
wa Maendeleo ya Mtoto, wakati wa maadhimisho ya Siku ya kupinga
ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu (mstari wa mbele katikati),
Mkuu wa wilaya ya Dodoma Dkt. Jasmine Tisekwa ( Kulia) na Muwakilishi
wa UNFPA, Bi Christine Mwanukuzi ( Kushoto) wakiwa katika picha ya
pamoja na wanachama wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
yanayopinga Ukeketaji Tanzania, wakati wa maadhimisho ya Siku ya kupinga
ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike.
Post a Comment