WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu kutoka nchi za Uturuki, Ireland na Uswisi pamoja na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti na mabalozi hao jana (Jumanne, Februari 23, 2016),
ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliwashukuru
mabalozi hao kwa kuja kujitambulisha rasmi na kwa pongezi walizokuja
kumpatia na kuahidi ushirikiano zaidi pamoja na nchi hizo.
Mapema jana, Waziri Mkuu alikutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez ambaye alimweleza
jinsi UNDP imekuwa ikisaidia programu za kukabiliana na maafa
(resilience), ukuaji wa uchumi, utawala bora na masuala ya jinsia.
Alisisitiza
haja ya Tanzania kuendeleza kampeni ya kupambana na ujangili na
kusisitiza kuwa Umoja huo una nia ya kusaidia utekelezaji wa Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Naye
Balozi wa Uturuki, Bibi Yesemin Eralp alimweleza Waziri Mku nia ya nchi
kuleta wawekezaji katika nyanja za kilimo, nishati, afya na ujenzi na
kusisitiza kuwa kuna haja ya kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwao
ili kuimarisha uhusiano uliopo.
“Tunao
uwezo wa kifedha na tunao uwezo wa kitaalamu na kiteknolojia.
Tukifungua viwanda hapa nchini, tunaweza kuongeza ajira kwa Watanzania,” alisema.
Naye
Balozi wa Ireland nchini, Bibi Fionnuala Gilsenan alimweleza Waziri
Mkuu jinsi ambavyo nchi yake imekuwa ikisaidia sekta za kilimo kupitia
mpango wa ASDP, bajeti ya Serikali na suala la lishe na urutubishaji wa
vyakula (food nutrition and fortification).
“Tulianza
na suala la kilimo na bajeti ya Serikali. Hivi sasa tunataka kusaidia
kwenye uelimishaji juu ya haki za wanawake, masuala ya uzazi wa mpango,
pamoja na kupambana na ndoa za utotoni,” alisema.
“Tumeamua
kupigia kelele suala la lishe na urutubishaji wa vyakula kwa sababu
lishe duni imechangia kwa kiasi kikubwa udumavu wa watoto wengi.
Tulipoanza tatizo hili lilikuwa limeenea kwa asilimia 46 kwa watoto
walio chini ya umri wa miaka mitano lakini sasa limepungua na kufikia
asilimia 36 hadi 38,” aliongeza.
Alimuomba
Waziri Mkuu Majaliwa alishikie bango suala hilo kwa Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya kote nchini kwani mtoto akishadumaa kimakuzi hata akili
yake pia inadumaa na tatizo lake haliwezi kurekebishwa kwa tiba yoyote
ile.
Naye
Balozi wa Uswisi nchini, Bibi Florence Mattli alimweleza Waziri Mkuu
nia ya nchi yake kudumisha ushirikiano na Tanzania ambao umedumu kwa
miaka 50 ili kukuza viwango vya uchumi na kuleta maendeleo kwa
Watanzania.
Alimweleza
Waziri Mkuu jinsi nchi yake imekuwa ikisaidia kundeleza nyanja za
kupambana na rushwa kupitia TAKUKURU na kampeni ya kusaidia kujenga
uelewa wa wananchi kupitia vyombo vya habari nchini.
Post a Comment