WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara ya ghafla kwenye kitengo cha
upimaji mafuta bandarini (Oil Flow Metres) na kukuta zimejaa kutu baada
ya kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano. Pia alitembelea mita za
kupimia mafuta zinazoendelea kujengwa Kigamboni.
Aidha,
Waziri Mkuu amempa saa nne tu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini
(WMA), Bi. Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini
aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita
na amletee barua hiyo ofisini kwake ifikapo saa 11 leo jioni.
“Nataka
unieleze ni kwa nini ulitoa maelekezo ya kufunga mita hizo, na kwa nini
jana uliamua kubadili uamuzi huo? Ni kwa nini umeamua kuchukua maamuzi
haya baada ya kupokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms) wakati mita
zimekaa bila kufanya kazi kwa miaka mitano? Ni kwa nini umeamua kufanyia
kazi ujumbe wa sms wakati unajua Serikali inafanya kazi kwa maandishi
rasmi?” alisema Waziri Mkuu.
“Umesema
mlikuwa mnatumia utaratibu wa kupima kwa kijiti. Huu hauna uhakika na
huwezi kutegemea taarifa ya mtu mwingine au kuingia kwenye meli ya mtu
na kuanza kuchukua vipimo hadi ujiridhishe. Nataka kujua ni kwa nini
mlikuwa na utaratibu wa ku-bypass mafuta ili yasipite kwenye mita za
kupimia mafuta? Ni kwa nini umetoa amri zianze kutengenezwa jana na siyo
mwaka 2012 au 2013?” alihoji Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu alisema mita hizo za Kurasini zilinunuliwa na Serikali kwa gharama
za dola za marekani milioni 1.2 (wakati huo) na haiwezekani kuacha
kuzitumia wakati watu wanachezea mifumo na kuongeza mianya ya kupoteza
mapato kwa Serikali. Ameagiza mita hizo zianze kufanya kazi mara moja.
Wazir
Mkuu alisema matumizi ya mita hizo yaliafikiwa na Serikali baada ya
kubaini upotevu mkubwa wa kodi kwenye mafuta yanayoingizwa nchini na
baada ya kuona hakuna tija ya kuendelea na ukadiriaji au kupokea taarifa
za waagizaji peke yao.
Waziri
Mkuu ambaye aliwasili Kurasini leo saaa 4: 30 asubuhi (Alhamisi,
Februari 11, 2016) kwenye kitengo hicho kilichopo Kurasini (Kurasini Oil
Jetty), alikagua mita hizo na kisha kwenda kukagua meli iliyokuwa
ikishusha mafuta bila kutumia mita hiyo ya kupima mafuta yanayopokelewa
kwa sababu mafundi walikuwa bado wanaendelea na ukarabati.
Akiwa
Kurasini, Waziri Mkuu alielezwa na Bibi Chuwa kwamba mita hizo zilianza
kufanyiwa ukarabati jana na leo asubuhi moja imekamilika ambayo ni ya
kupokelea mafuta ya petroli. Ya dizeli ilikuwa inafunguliwa na mafundi
na kukutwa imejaa kutu sababu ya kutotumika kwa muda mrefu.
“Hii ya dizeli imefunguliwa leo na ile ya mafuta ya kula, haijawahi kufanya kazi tangu ilipofungwa mwaka 2011,” alielezwa Waziri Mkuu na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei.
Alipoulizwa
ni kwa nini aliamua kuzifungia mita hizo ziisifanye kazi, Bi. Chuwa
alijibu kuwa alifikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kwamba
zinawapunja wateja. Hata hivyo, hakufafanua ni wateja gani au wa aina
gani.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea na kukagua mita mpya
za kupimia mafuta ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu
dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).
Akiwa
hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba ujenzi huo ambao ulianza miezi nane
iliyopita, unatarajiwa kukamilika ifikapo katikati ya mwezi Machi, 2016.
“Tunajitahidi kazi hii ikamilike ifikapo katikati ya mwezi ujao,”
alisema Eng. John Bura, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BQ Contractors
Ltd ambayo inasimamia ujenzi wa mita hizo.
Vilevile,
Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka
bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya
kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko
Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia bainaya Serikali na kampuni ya Oryx
Energies.
Katika
ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la
moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini
hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye
maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Natoa mwezi mmoja hili bomba liondolewe kwenye mfumo huu na kama yapo mabomba mengine pia yaondolewe,”
alisema huku akionyesha karatasi iliyokuwa mfukoni kwake yenye mchoro
unaobainisha kuwa kuna bomba jingine la inchi 10 limeungwa kinyemela
kwenye bomba kuu.
“Kila
mmoja anapaswa aje kuchukua pale kwenye manfold ili tujue nani kachukua
nini. Msajili wa Hazina hili ni eneo lako na wewe unamiliki TIPER kwa
asilimia 50, hebu simamia hili. Ninyi TPA leteni mapendekezo yenu
Serikalini ili tuone tunaweza kudhibiti vipi vitendo kama hivi,” alisema Waziri Mkuu.
Pia
alimtaka Msajili wa Hazina, Bw. Lawrence Mafuru awasiliane na
Mwanasheria Mkuu ili waangalie upya mkataba na umiliki wa matenki hayo
uwe chini ya Serikali kwa asilimia 100 ili mafuta yanayoagizwa na Wakala
wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency)
yaweze kuhifadhiwa huko.
Mapema,
Waziri Mkuu ambaye alifuatana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alikagua eneo la manfold ya Mamlaka
ya Bandari iliyopo Kigamboni na kukuta ni kampuni nne tu zenye matenki
Kigamboni ambazo zinachukua mafuta yao hapo.
Kampuni
hizo ni HASS, WORLD OIL, LAKE OIL na MOIL. TIPER haikutaka kufuata
mfumo huo licha ya kuwa nafasi ya kufanya hivyo ipo. Kampuni nyingine
zenye matenki yake nchi kavu, zinachukulia mafuta kwenye manfold ya
Kurasini.
Post a Comment